Mkunga apiga kambi kwa wakimbizi ili kuepusha vifo vya wajawazito - Chad
Nchini Chad, taifa lililoko kaskazini-kati mwa Afrika mkunga mmoja amehamia kwa muda katika kambi ya wakimbizi ili kuhakikisha wajawazito wanapata huduma bora kabla na baada ya kujifungua kama njia mojawapo ya kuepusha vifo vya wajawazito na watoto wachanga.
Naam, taarifa yangu hii ni kwa hisani ya video ya shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, UNFPA hapa Chad, ikianza kwa kutuonesha mkunga huyo Florence Denemadji akitembea katikati ya mahema ya wakimbizi.
UNFPA inasema zaidi ya watu 13,000 nchini Chad, wengi wao wakiwa ni wajawazito wamefurushwa makwao kutokana na mafuriko yaliyokumba nchi nzima. Sasa janga la tabianchi linaongeza hatari, ya sio tu ukatili wa kijinsia na ubakaji, bali pia vifo vya wajawazito.
Florence ambaye yuko kwenye eneo hili kwa miezi mitatu sasa, anaingia ndani ya hema moja, na kumkuta mama na mtoto mchanga. Florence anasema.
“Natoa huduma wakati wa majanga na dharura. Naelimisha akina mama na kuwapatia mafunzo juu ya malezi ya watoto wao, ikiwemo kuwanyonyesha bila kuwapatia kitu kingine. Tunawaangalia vizuri hawa akina mama. Na kutokana na huduma za UNFPA, hakuna vifo vya wajawazito.”
Akatoka hema hili na kuingia kwenye hema lingine, ambamo tunakutana na Chancelin Milamen, mama mkimbizi huyu akitoa ushuhuda wa huduma ya Florence, huku akiwa amembeba mtoto wake.
“Tulipofika hapa, nilikuta wakunga. Walinipima na kunihudumia hadi uchungu ulipoanza. Nilijifungua mwanangu mikononi mwao.”
Nchini Chad, taifa lililoko kaskazini-kati mwa Afrika mkunga mmoja amehamia kwa muda katika kambi ya wakimbizi ili kuhakikisha wajawazito wanapata huduma bora kabla na baada ya kujifungua kama njia mojawapo ya kuepusha vifo vya wajawazito na watoto wachanga. Taarifa ya Evarist Mapesa inafafanua zaidi.