Raia wa Mali walioko ughaibuni waonesha mfano bora wa kuwekeza nyumbani
Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD kwa kushirikiana na wadau na kupitia msaada wa Muungano wa Ulaya unasaidia raia wa Mali wanaoishi ughaibuni kuwekeza kwa ufanisi nyumbani Mali.
Wamefanya hivyo kwa kuwasaidia kuanzisha Ciwara Capital, kampuni ya uwekezaji inayomilikiwa na raia wa Mali na sasa wanasaidia wakulima wa mpunga nchini Mali kuimarisha na kuongeza uzalishaji wa mpunga, ikiwemo eneo la Mopti ambalo limekuwa likikabiliwa na ukosefu wa usalama na hivyo wakulima kugubikwa na umaskini.
Mfumo huu unadhihirisha kuwa badala ya waafrika kutuma dola bilioni 55 kila mwaka nyumbani kusaidia familia, fedha hizo zinaweza kuwekezwa kwenye miradi endelevu.
Makala hii inatupeleka Mopti, mji mkuu wa jimbo la Mopti lililoko katikati mwa taifa la Mali. Umsikiaye ni Ibrahima Samassekou, mkulima wa mpunga akiwa shambani mwake akisema mwaka huu tulipata mafuriko na hivi karibuni tulipata joto kali.
Vyote hivyo matokeo ya mabadiliko ya tabianchi, vimekuwa na madhara kwenye kilimo cha mpunga. Kama hiyo haitoshi hata kile walichokuwa wanavuna walikuwa hawana uhakika wa soko. Lakini nuru ikaanza kuonekana.
“Wamekuwa wanatupatia pembejeo kiasi na sisi kwa upande wetu tunawapatia hakikisho la kuwauzia kiasi fulani cha mazao yetu.”
Unaweza kujiuliza hao ni akina nani? Hao ni raia wa Mali wanaoishi ughaibuni ambao waliona badala ya kutuma tu fedha nyumbani kwa ndugu na jamaa ni vema kuanzisha mfuko wa uwekezaji, Ciwara Capital na kuwekeza kwenye mradi utakaokuwa na faida kwa jamii kubwa zaidi.
Moussa Bagayoko ni Muasisi mwenza na Afisa Mtendaji Mkuu wa Ciwara Capital.
“Lengo kwa kweli ni kujengea uwezo na kuinua kampuni binafsi Afrika kwa kupatia teknolojia na fedha ambazo walio ughaibuni wanaweza kuhamasisha na kushiriki pia kwenye maendeleo ya bara hili.”
Sasa Ciwara Capital imewekeza kwenye kampuni ya SOPROTRILAD iliyoko Mopti, Mali inayolima, inachakata na kuuza mchele. SOPROTRILAD inashirikiana na zaidi ya vyama 160 vya ushirika wa kilimo ikiwemo cha akina Ibrahima, ikisaidia wakulima wadogo zaidi ya 3,000 nchini Mali.
Hii inawezesha Ibrahima na wenzake kuwa na uhakika wa zao la mpunga wakati wowote ule tofauti na zamani.
Oumarou Amadou Sankaré, mwakilishi wa SOPROTRILAD anasema.
“Tunajenga kiwanda kipya, hivyo tutahitaji mpunga mwingi zaidi. Tutawasiliana na wakulima wengi, na hii itapunguza njaa na kitendo cha watu kuhama vijijini kwani hapa kuna kazi. Tunajaribu kuwafundisha vijana kuhusu mbinu za kilimo ili wabakie hapa walime. Kilimo hakimtupi mtu.”
SOPROTRILAD kwa msaada kutoka Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD umepatia wakulima na vyama vya ushirika mbinu za kisasa za kilimo cha mpunga kinachopunguza matumizi ya maji na mbolea, kinatoa kiwango kidogo cha hewa chafuzi na kuongeza afya ya udongo, matumizi kidogo ya mbegu, lakini kiwango kikubwa cha mavuno. Miongoni mwa mbinu hizo ni pamoja na mfumo mpya wa kilimo cha mpunga uitwao System of Rice Intensification au SRI. Mkulima Ibrahima akafafanua faida yake.
“Mfano katika eneo la robo eka, tulikuwa tunapanda kilo 13 za mbegu. Lakini kupitia mfumo huu mpya tunatumia mbegu kilo 2 tu au 3. Tunatumia kiwango kidogo cha maji, hii ina maana unaokoa mafuta ya kusukuma pampu ya maji. Kwa robo eka tulivuna magunia kati ya 20 hadi 25 ya mpunga lakini na mfumo mpya magunia hadi 34. Ingawa mbinu inahitaji kazi nyingi lakini ina manufaa zaidi.”
Katika baadhi ya matukio wawekezaji kutoka ughaibuni wamekuwa wakikatishwa tamaa na matumizi holela ya fedha zao au miradi kutoenda walivyotarajia. Lakini Sankare ambaye ni Mwakilishi wa SOPROTRILAD akawa na neno kwa Ciwara Capital.
“Inaonesha kwamba hawa raia wa Mali wanaoishi ughaibuni wanataka kusaidia nchi yao. Hawa ni wazalengo, hawajatusahau. Tuwahakikishie kwamba tutatumia vema fedha zao kama watakavyo na pale ambapo itahitajika.”
Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD kwa kushirikiana na wadau na kupitia msaada wa Muungano wa Ulaya unasaidia raia wa Mali wanaoishi ughaibuni kuwekeza kwa ufanisi nyumbani Mali.
Wamefanya hivyo kwa kuwasaidia kuanzisha Ciwara Capital, kampuni ya uwekezaji inayomilikiwa na raia wa Mali na sasa wanasaidia wakulima wa mpunga nchini Mali kuimarisha na kuongeza uzalishaji wa mpunga, ikiwemo eneo la Mopti ambalo limekuwa likikabiliwa na ukosefu wa usalama na hivyo wakulima kugubikwa na umaskini.
Mfumo huu unadhihirisha kuwa badala ya waafrika kutuma dola bilioni 55 kila mwaka nyumbani kusaidia familia, fedha hizo zinaweza kuwekezwa kwenye miradi endelevu. Je ni kwa vipi, Assumpta Massoi anafafanua kwenye makala hii iliyoandaliwa na IFAD.