10 DESEMBA 2024
Pakua
- Baada ya serikali ya Bashar Al-Assad kupinduliwa na kuibuka kwa taarifa za baadhi ya nchi duniani kuanza kusitisha mchakato wa kushughulikia maombi ya Wasyria waliokuwa wameomba hifadhi kuokoa usalama wa maisha yao pindi hali ilipokuwa tete nchini mwao, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) linaendelea kutoa wito kwa mataifa yote kufungua milango, kuwapa hifadhi na ulinzi raia wa Syria wanaotafuta usalama. UNHCR imeahidi pia mara tu hali ya Syria itakapokuwa wazi zaidi, itatoa mwongozo kuhusu mahitaji ya ulinzi kwa Wasyria walioko hatarini.
- Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limekaribisha mchango wa dola za Marekani milioni 22 kutoka shirika la Korea Kusini la Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa (KOICA) ili kuimarisha mnepo kwa tabianchi na uhakika wa chakula kwa wakulima wadogo, wafugaji na makundi yaliyoko pembezoni nchini Kenya, Somalia na Sudan Kusini. Vituo vya utabiri wa hali ya hewa vinatabiri hali ya La Niña mashariki mwa Pembe ya Afrika na uwezekano wa kupunguza mvua katika kipindi hiki
- Na walinda amani wa kikosi cha 11 cha Tanzania -TANZBATT-11 kinachohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO jimboni Kivu Kaskazini wametunukiwa nishani ya umoja wa mataifa ikiwa ni alama ya kufanya kazi kwa utii,uhodari na uaminifu. Miongoni mwao ni Private Selina Kisemvule.
- Katika mashinani ikiwa ni siku ya mwisho ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, fursa ni yake Rais Nangolo Mbumba wa Namibia ambaye kupitia ukurasa wa X wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi na Idadi ya Watu, UNFPA anawahimiza wananchi na dunia nzima kwa jumla kusimama kidete ili kutokomeza unyanyasaji wa kijinsia.
Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!
Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
9'58"