Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN na wadau wazindua ombi la dola bilioni 47 kwa ajili ya mwaka 2025

UN na wadau wazindua ombi la dola bilioni 47 kwa ajili ya mwaka 2025

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ikizindua Ripoti ya Kimataifa ya mahitaji ya Kibinadamu (GHO) kwa mwaka ujao wa 2025 imetangaza ombi la ufadhili kwani takriban watu milioni 305 duniani kote watahitaji msaada wa kibinadamu katika mwaka ujao. 

Ombi hilo linataka dola bilioni 47 za kimarekani lililotangazwa leo Desemba nne jijini Geneva Uswisi ni kwa ajili ya kutoa msaada wa kuokoa maisha katika nchi 33 na kanda tisa zinayohifadhi wakimbizi.

"Katika ulimwengu ulioko katika matatizo, walio hatarini zaidi, watoto, wanawake, watu wenye ulemavu na maskini - wanalipa bei kubwa zaidi," Tom Fletcher, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, amesema na kuongeza  kwamba, "lazima turekebishe upya uhusiano wa ulimwengu na watu wenye uhitaji mkubwa," Bwana Fletcher anahimiza. "Sauti zao na uharaka lazima ziwe kiini cha mwitikio wetu. Tunahitaji kiwango kipya cha mshikamano wa kimataifa ili kufadhili kikamilifu rufaa hizi, na hatua za kijasiri za kisiasa kudumisha sheria za kimataifa. Jumuiya ya kibinadamu iko tayari kutoa - kwa manusura waliochoshwa na vita, familia iliyofurushwa, mtoto mwenye njaa. Ni lazima tutengeneze na tushinde upya hoja kwa ajili ya ubinadamu.”

Migogoro ya kivita inaongezeka mara kwa mara na kwa ukatili, na kulazimisha karibu watu milioni 123 kukimbia makazi yao. Maafa yanayosababishwa na tabianchi yanaharibu jamii, mifumo ya chakula inayoharibu na kusababisha watu wengi kuhama makazi yao. Wakati huo huo, migogoro ya zamani bado haijatatuliwa, huku ombi la wastani la kibinadamu sasa likichukua muongo mmoja.

GHO ya 2025 inaelezea mipango ya hatua iliyopewa kipaumbele kwa uangalifu, ikiunganisha zaidi ya wadau 1,500 wa kibinadamu ili kutoa msaada muhimu kwa watu milioni 190 duniani. Licha ya ukarimu wa muda mrefu wa wafadhili, uhaba wa fedha unaendelea. Kufikia Novemba 2024, ni asilimia 43 tu ya ombi la dola bilioni 50 kwa mwaka huo ilikuwa imepatikana.

Madhara ya ufadhili mdogo ni makubwa. Mwaka 2024 ulishuhudia kupungua kwa asilimia 80 kwa msaada wa chakula nchini Syria; kupunguzwa kwa huduma za ulinzi nchini Myanmar; kupungua kwa msaada wa maji na vifaa vya kujisafi kwa Yemen inayokumbwa na kipindupindu; na njaa inayoongezeka nchini Chad.

Hata hivyo, kizuizi kimoja muhimu zaidi cha kusaidia na kulinda watu katika migogoro yenye kutumia silaha ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu. mwaka 2024 tayari ni mwaka mbaya zaidi kwa wafanyikazi wa misaada ya kibinadamu, ikipita idadi ya vifo vya mwaka jana ya watu 280. Idadi kubwa ya waliopoteza maisha ni wafanyakazi wa misaada ya kitaifa.

Hata hivyo, licha ya changamoto hizi, mashirika ya kibinadamu yalifikia karibu watu milioni 116 mwaka 2024, yakitoa huduma muhimu za chakula, malazi, afya, elimu na ulinzi.

Pakua

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ikizindua Ripoti ya Kimataifa ya mahitaji ya Kibinadamu (GHO) kwa mwaka ujao wa 2025 imetangaza ombi la ufadhili kwani takriban watu milioni 305 duniani kote watahitaji msaada wa kibinadamu katika mwaka ujao. Selina Jerobon na maelezo zaidi.

Audio Credit
Selina Jerobon
Audio Duration
2'3"
Photo Credit
IOM/Léo Torréton