Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP: Bila msaada wa kibinadamu Wasudan watakufa kwa njaa

WFP: Bila msaada wa kibinadamu Wasudan watakufa kwa njaa

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, (WFP) leo kwa mara nyingine tena limetahadharisha kwamba bila msaada wa kibinadamu nchini Sudan, mamia ya maelfu wanaweza kufa kwa njaa. 

Vita vya kikatili nchini Sudan vimesababisha janga kubwa zaidi la njaa duniani, imeandika WFP katika ukurasa wake wa X leo Oktoba 28 na kufafanua zaidi kwamba mtu mmoja kati ya watu wawili nchini humo anatatizika kupata mlo kila siku.

WFP inaeleza kuwa njaa imethibitishwa Kaskazini mwa Darfur na mahitaji ya kibinadamu ni makubwa sana.

Kabla ya taarifa hii ya leo ya WFP, jana kupitia pia ukurasa wa mtandao wa X, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Cindy McCain ambaye hivi karibuni alikuwa Sudan mojawapo ya maeneo yenye njaa zaidi duniani, ambapo watu milioni 25 wanakabiliwa na njaa kali ameandika kwamba WFP iko Sudan inatoa msaada wa kuokoa maisha lakini wanahitaji kwa haraka mambo matatu ambayo ni kuwafikia watu ili kuwasaidia, misaada kuweza kupita katika kila kivuko na usaidizi zaidi wa kimataifa kwa Wasudani walio katika mazingira hatarishi.

Kwa miaka mingi, Sudan imekuwa ikisumbuka na migogoro. Mgogoro wa hivi karibuni zaidi, ulioanza Aprili mwaka jana 2023, umezua janga baya zaidi duniani la watu kuhama makwao na janga kubwa zaidi la njaa duniani linalosambaa Sudan, Sudan Kusini na Chad.

Audio Credit
Selina Jerobon
Audio Duration
1'35"
Photo Credit
© WFP/World Relief