Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

12 SEPTEMBA 2024

12 SEPTEMBA 2024

Pakua

Hii leo jaridani mada kwa kina inayotupeleka nchini Tanzania, kulikofanyika mashauriano kuhusu mkutano wa zama zijazo, ambapo baadhi ya washiriki wameeleza walichojadili na walichopendekeza. Pia tunakuletea muhtasari wa habari na maana ya neno “KILIWAZO”.

  1. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X amelaani vikali tukio la jana huko Gaza ambapo vikosi vya anga vya Israel vilishambulia makazi ya wakimbizi wa ndani wapatao 12, 000. Katika shambulio hilo wafanyakazi 6 wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA walifariki dunia na kufanya tukio hilo kuwa lenye vifo vingi zaidi vya wafanyakazi wa UNRWA katika tukio moja.
  2. Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) na wadau wake, jana Septemba 11 huko Gaza wamefanikiwa kuhamisha wagonjwa 97 na watu wengine 155 wenye majeraha makubwa zaidi. Katika unaotajwa kuwa uhamishaji mkubwa wa wagonjwa tangu ule wa Oktoba 2023 wagonjwa walisafirishwa kupitia Kerem Shalom hadi Uwanja wa Ndege wa Ramon nchini Israel kwa safari ya kuelekea Abu Dhabi, Falme za Kiarabu.
  3. Tukisalia huko Gaza, takribani robo moja au watu elfu ishirini na mbili na mia tano ya wale waliojeruhiwa huko Gaza kufikia Julai 23 wanakadiriwa kuwa na majeraha ambayo yatabadilisha kabisa maisha yao na kwa hivyo wanahitaji huduma za uangalizi sasa na hata kwa miaka ijayo. Hiyo ni kwa mujibu wa uchambuzi uliotolewa leo na WHO.
  4. Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili leo fursa ni yake mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA anafafanua maana ya neno “KILIWAZO”.

Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu! 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
9'59"