Mkutano wa ufadhili wapata msaada wa fedha wa dola milioni 610 kwa ajili ya Ethiopia
Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Kutoa ahadi kwa ajili ya ufadhili wa kukwamua hali ya Kibinadamu nchini Ethiopia uliokamilika jana mjini Geneva, Uswisi umetangaza kwamba wafadhili 20 wametangaza msaada wa kifedha wa Dola za Marekani milioni 610 angalau kuhakikisha misaada kwa miezi michache ijayo.
Mkutano huo uliolenga kukusanya dola bilioni 1 za kimarekani kwa ajili ya miezi mitano ijayo, ulikuwa umeandaliwa kwa pamoja kati ya Umoja wa Mataifa, Serikali ya Ethiopia na Uingereza, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa masuala ya kibinadamu.
Mara tu baada ya mkutano huo Naibu Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu na Masuala ya Dharura OCHA, Joyce Msuya, aliwashukuru wafadhili hao na kusema kuwa huo ni mwanzo tu na matumaini ni kuendelea na kuongeza msaada kwa mwaka mzima.
Dharura ya kibinadamu nchini Ethiopia imekuwa ikiongezeka kupitia mizunguko ya ukame na mafuriko, na migogoro. Ukosefu wa uhakika wa chakula na utapiamlo unatarajiwa kufikia kiwango cha juu kwa watu milioni 10.8 wakati wa msimu wa muwambo kati ya mwezi Julai na Septemba.
Viwango vya utapiamlo katika sehemu za Afar, Amhara, Tigray na mikoa mingine vinatia wasiwasi mkubwa na vinaendelea kuwa vibaya zaidi. Wakati huo huo, migogoro katika Tigray na mikoa mingine imeharibu maelfu ya shule, vituo vya afya, mifumo ya maji na miundombinu mingine ya jamii.
Mama huyu ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiusalama ni wa eneo la Afar, mashariki mwa Ethiopia ambako pia kumeathiriwa na mafuriko anapaza sauti akisema, “Ninataka kulea na kusomesha watoto wangu vizuri. Nawatakia watoto wangu mema.”
Umoja wa Mataifa na wadau wa kibinadamu wanaunga mkono mwitikio wa kitaifa wa kuongeza msaada wa kuokoa maisha kwa watu milioni 15.5, na msaada wa chakula kwa watu milioni 10.4 nchini humo Ethiopia. Kwa mwaka mzima, ili mpango huo ufanikiwe unahitaji dola za Marekani bilioni 3.24.