Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Saratani ya shingo ya kizazi inatibika ikigundulika mapema – WHO

Saratani ya shingo ya kizazi inatibika ikigundulika mapema – WHO

Pakua

Mwezi huu wa januari umetangazwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya WHO kuwa ni mwezi wa kujenga ufahamu kuhusu ugonjwa wa Saratani ya shingo ya Kizazi, nami nimemualika mwenzangu Leah Mushi hapa studio ambaye amefuatilia kwa kina suala hilo kupitia wavuti wa WHO.

Swali: Leah kwanza tueleze lipi hasa WHO wanalotaka wadau wafanye?

Jibu: WHO inahamasisha mambo makuu 3 mosi, kutoa taarifa kuwa kuna ugonjwa huo, pili kuhimiza uchunguzi na tatu kuhamasisha chanjo. 

Swali: Tuanze na hilo la kwanza taarifa za ugonjwa huo?

Jibu: Assumpta ningependwa kuwajuza wasikilizaji wetu kuwa 90% ya wanaougua saratani ya shingo ya kizazi ni kutoka nchi masikini na viwango vya juu vya vifo ni kutoka Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, Amerika ya Kati na Kusini-Mashariki mwa Asia. 

Swali: Mtu anapataje saratani hii?

Jibu: WHO inasema virusi aina ya Human Papiloma (HPV) ambayo huambukizwa kwa njia ya zinaa ndio chanzo, mgonjwa asipopata matibabu au maambukizi ya mara kwa mara ya virusi hivyo vya HPV yanaweza kusababisha seli zisizo za kawaida kukua, ambazo zitaendelea kukua na kuwa saratani.

Lakini pia wagonjwa wa UKIMWI wapo katika hatari mara 6 zaidi ya kupata saratani ya shingo ya kizazi. 

Swali: Mtu anawezaje kujikinga?
Jibu: Kubwa ni kupata chanjo ya HPV na inaanza kutolewa kwa wasichana katika umri ambao bado hawajaanza kujamiiaa ndio maana inahimizwa kutolewa kuanzia umri wa miaka 9 mpaka 14.

Pia kufanya uchunguzi wa kizazi, mwanamke kuanzia umri wa miaka 35 na kuendelea anapaswa angalau mara 2 kwa mwaka kwenda kufanya uchunguzi. 

Swali: Tiba sasa ni nini?

Jibu: ukigundulika tiba ni zile za wagonjwa wa saratani kama vile upasuaji, tiba ya mionzi na tibakemikali ili kutoa huduma pamoja na udhibiti wa maumivu.

Audio Credit
Leah Mushi/Assumpta Massoi
Sauti
1'59"
Photo Credit
Pan American Health Organization