Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN: COP28 yafunga pazia kwa muafaka wa kuanza kutokomeza mafuta kisuskuku

UN: COP28 yafunga pazia kwa muafaka wa kuanza kutokomeza mafuta kisuskuku

Pakua

Hatimaye mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP28, leo umekunja jamvi mjini Dubai huko Umoja w Falme za Kiarabu (UAE) kwa muafaka ambao Umoja wa Mataifa unasema unatoa ishara ya kuanza kutokomezwa kwa mafuta kisukuku au Fossil Fuels, ingawa baadhi ya nchi za visiwa vidogo vinavyoendelea ikiwemo Samoa zinaona muafaka huo hautoshelezi kuwalinda kikamilifu dhidi ya tabianchi.

Ni Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi Simon Stiell akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya makubaliano kufikiwa akisema ingawa hawafungua ukurasa mpya kabisa wa kutokomeza mafuta kisukuku Dubai lakini makubaliano hayo yanatoa ishara ya kuanza utokomezaji wa mafuta hayo ambayo ni kichocheo kikubwa cha mabadiliko ya tabianchi. 

Stiel amesema makubaliano hayo  yameweka msingi wa mpito wa haraka, wa haki na usawa, unaounga mkono kupunguzwa kwa kiasi kikubwa kwa uzalishaji wa hewa chafuzi na kuongezwa kwa ufadhili.”

Amesisitiza kuwa “sasa serikali na sekta ya biashara wanahitaji kugeuza ahadi hizi kuwa matokeo halisi ya ya uchumi, bila kuchelewa.

Akitoa kauli yake baada matokeo ya mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema "licha ya tofauti nyingi, ulimwengu unaweza kuungana na kukabiliana na changamoto ya janga la mabadiliko ya tabianchi. Ushirikiano wa kimataifa unasalia kuwa tumaini bora la ubinadamu." 

Kwa wale waliopinga kuainisha wazi utokomezaji wa nishati ya mafuta kisukuku katika waraka wa COP28, amesema "utokomezaji wa mafuta kisukuku haiwezi kuepukika watake wasitake. Hebu tutumaini kwamba hautachelewa sana. "

Na mgawanyiko wa matokeo hayo ulikuwa bayana hususan kwa visiwa vidogo vinavyoendelea kama Samoa ambayo haikuficha hisia zake kuhusu matokeo na Stiel amekiri hilo akisema, tumesikia wasiwasi wa Samoa na mataifa yote ya visiwa ambayo yameweka wazi kwamba muafaka huu hautoshelezi kulinda watu wao na sayari. Ukweli kwamba ndio walioshangiliwa zaidi ni ishara tosha kwamba hisia zao zinaungwa mkono na wengi.”

Washiriki kutoka nchi 199 na takriban pande 200 wamejadiliana Dubai kwa wiki mbili kwa lengo la kudhibiti athari za madiliko ya tabianchi na hasa kuhakikisha joto la duniani haliongezeki zaidi ya nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'47"
Photo Credit
UNFCCC/Kiara Worth