Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres kwa washiriki COP28: Epukeni majawabu ya kutia moyo bila ufanisi

Guterres kwa washiriki COP28: Epukeni majawabu ya kutia moyo bila ufanisi

Pakua

Mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28 ukifikia ukingoni huko Dubai, Falme za Kiarabu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka washiriki waepuke msemo wa “Funika kombe mwanaharamu apite,” na badala yake waje na majawabu ya kina na ya kijasiri ili lengo la kutozidi kwa nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha selsiyasi liweze kufikiwa. 

Katibu Mkuu Guterres akizungumza na waandishi wa habari hii leo huko Dubai, Falme za Kiarabu amewakumbusha wasongeshaji wa majadiliano hayo kwenye COP28 kuwa mkutano unakunja jamvi kesho lakini bado kuna mapengo makubwa ya kuzibwa.  

Ni wakati wa kusaka kulegeza misimamo ili kupata majawabu, anasema Guterres, akiongeza kuwa misimamo hiyo ilegezwe bila kupuuza sayansi au kupuuza umuhimu wa kuwa na matamanio makubwa. Anasema katika dunia iliyomeguka na kugawanyika, COP28 inaweza kudhihirisha kuwa ushirikiano wa kimataifa ndio tumaini letu bora la kutatua changamoto za dunia. 

Ndio hapo Katibu Mkuu akataja maeneo mawili ambayo anasihi pande husika kwenye mkutano huo kuyapatia kipaumbele: Mosi kupunguza utoaji wa hewa chafuzi na kuhakikisha kuna majawabu yanayopatia haki tabianchi. 

Katibu Mkuu anasema Uhakiki wa kimataifa lazima uwasilishe mpango wa wazi wa kuongeza nishati rejelezi, kuongeza maradufu nishati fanisi, na mpango mmoja wa kushughulikia vyanzo vya janga la tabianchi ambavyo ni uzalishaji na utumiaji wa nishati kisukuku. 

“Ametamatisha mkutano wake kwa kusema lazima COP28 imalizike kwa kuendeleza azma ya kudhibiti kiwango cha joto kisizidi nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi kama ilivyopitishwa na Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya tabianchi mwaka 2015. 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Sauti
1'56"
Photo Credit
COP28/Christopher Pike