Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres aonya kwamba kifanyikacho Antarctica sasa hakisalii tena huko kinasambaa

Guterres aonya kwamba kifanyikacho Antarctica sasa hakisalii tena huko kinasambaa

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye yuko ziarani katika eneo la ncha ya kusini mwa dunia, Antarctica amesema eneo hilo limekuwa likijulikana kama eneo lenye manufaa makubwa lakini lililosahaulika, lakini sasa limeamshwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. 

Kauli hiyo imekuwa na mashiko kwa miongo kadhaa kwa msingi kwamba eneo la ncha ya kusini mwa dunia liko mbali na wengi, lakini sasa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa katika ziara ya siku tatu kwenye eneo hilo amejionea akiwa ameambatana na Rais Gabriel Boric wa Chile jinsi kile kinachofanyika maelfu ya maili kinaathiri eneo hilo, na halikadhalika kifanyikacho eneo hilo hakisalii tena eneo hilo kama ambavyo awali watu walidhania. 

Ametembelea kisiwa cha Kopaitic ambacho ni makazi ya ndege wa baharini aina ya Kiwi na kuona ni kwa jinsi gani mabadiliko ya tabianchi yameathiri eneo hilo. 

Mathalani nishati kisukuku ambayo ni mafuta yatokanayo na upasuaji na uchomaji wa miamba! Katibu Mkuu amesema uchafuzi utokanao na shughuli hiyo husababisha joto kwenye sayari ya dunia, vivyo hivyo Antarctica.  

Kielelezo ni ongezeko la joto kwenye baharí kusini mwa dunia ambalo limechochea mkondo joto baharini, El Nino unaosababisha mvua, mafuriko na joto kupindukia.  

Sasa kwa viongozi na washiriki wa mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP28 huko Dubai mambo matatu yazingatiwe: Mosi, wachukue hatua wahakikishe kiwango cha joto duniani hakizidi nyuzijoto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi; Pili, walinde binadamu dhidi ya zahma ya tabianchi na tatu waondokane na nishati kisukuku.  

Guterres amesema tusiache matumaini yote ya sayari endelevu yayoyome.  

Baadaye leo akiwa na Rais Boric watatembelea kituo cha Frei huko huko Antarctica na kesho Jumamosi atatembelea kituo cha wanasayansi cha Profesa Julio Escudero kupata taarifa kutoka kwa wanasayansi. Atarejea New York, Jumapili. 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'2"
Photo Credit
UN Photo/Mark Garten