Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

31 OKTOBA 2023

31 OKTOBA 2023

Pakua

Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina na leo tunabisha hodi nchini Kenya ambako hivi karibuni kumefanyika mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi ulioandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na ueneaji wa hali ya jangwa UNCCD ukishirikisha wadau wengine, kukijadili ni jinsi gani ya kuzishirikisha jamii kwanza kupunguza athari na gharama zinazoletwa na hali ya jangwa na pili kuwajengea mnepo wananchi dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Tuanluetea pia habari kwa ufupi zikiwemo za machafuko Gaza, afya nchini Sudan na ujumbe wa Katibu Mkuu wa kuhusu siku ya Miji Duniani. Mashinani tunakupeleka huko Port-au-Prince makao makuu ya taifa la Haiti, kulikoni?  

1. Gaza imegeuka "makaburi" ya watoto, kwani maelfu wameuawa kufuatia mashambulizi yanayofanywa na Israel huku zaidi ya Watoto milioni moja wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa mahitaji muhimu na maisha yao ya baadaye yakikabiliwa na kiwewe, amesema Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na dharura, OCHA, Martin Griffiths kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa X, hii leo. 

2. Dkt Ni’ma Saeed Abid ambaye ni Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) nchini Sudan, leo ameripoti kuwa Mfumo wa afya nchini humo umezidiwa kiasi cha kufikia hatua mbaya huku mahitaji yakiongezeka kutokana na milipuko ya magonjwa, utapiamlo, na kuongezeka kwa wagonjwa wenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambao hawajatibiwa mathalani wenye kisukari, shinikizo la damu, saratani, magonjwa sugu ya kupumua na figo. Kidogo Habari njema ni kuwa WHO Sudan inajiandaa kupokea chanjo ya matone dhidi ya kipindupindu kutoka kwa ICG ambalo ni Kundi la kimataifa la kuratibu usambazaji wa chanjo nyakati za dharura linachoundwa na WHO, UNICEF na wadau wao. 

3. Na ikiwa leo ni Siku ya Miji Duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake mahususi kwa siku hii ametoa wito kwamba, ‘tunapoadhimisha Siku ya Miji Duniani, tuazimie kufanya kazi pamoja kwa ajili ya maeneo ya mijini ambayo si tu ni injini za ukuaji, bali vinara wa uendelevu, mnepo, na ustawi kwa wote. Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi Duniani (UN Habitat), Maimunah Mohd Sharif akisisitiza Kaulimbiu ya mwaka huu, Kufadhili Mstakabali wa Miji Endelevu kwa wote, amesema unahitajika mfumo mpya wa ufadhili kwa ajili ya maendeleo endelevu ya miji na kwamba pia inahitajika kuwekeza katika upangaji jumuishi na kuongeza kasi ya kuyafanya makazi na nyumba kuwa haki ya binadamu.

4. Mashinani tunakupeleka huko Port-au-Prince makao makuu ya taifa la Haiti kumsikia Duvernise Altema akieleza maishi wanayoishi baada ya kulazimishwa kuyahama makazi yao kutokana na mzozo unaoendelea nchini humo. 

Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
11'38"