Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wenyeji Baringo nchini Kenya wanufaika kufuatia mradi wa maji wa WFP

Wenyeji Baringo nchini Kenya wanufaika kufuatia mradi wa maji wa WFP

Pakua

Uhakika wa upatikanaji wa maji ni moja ya suluhisho za kupambana na mabadiliko ya tabianchi hususan katika maeneo yanayokabiliwa na ukame. Nchini Kenya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani WFP kwakushirikiana na serikali wamewezesha wananchi wa kaunti ya Baringo kuondokana na adha ya maji. 

Kwa miaka takriban 40 wananchi wa Kaunti ya Baringo nchini Kenya wamekuwa wakitaabika na uhaba wa maji kutokana na ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Hali hiyo imewafanya wananchi hao kuwa tegemezi wa chakula kwa kwakuwa wamekosa maji ya kulisha mifugo yao na kilimo. 

Kutokana na adha hiyo WFP kwa kushirikiana na wadau wake na serikali ya Kenya imetekeleza mradi wa kuchimba visima mradi ambao Naibu gavana wa kaunti ya Baringo Felix Kimaiyo anasema unaenda kubadili maisha ya wananchi. 

“Mradi huu utakuwa muhimu sana kwa sababu unaenda kugusa maisha ya watu hawa na kuweza kupunguza maswala mengi na kuhakikisha kuwa eneo hili kuna uhakika wa upatikanaji wa chakula”

Naam, na WFP mpaka sasa imefanikisha kuchimba visima 74 na vingine 22 vikiendelea kuchimvwa. Na mabadiliko yanaonekana kwani mifugo imepata maji, kilimo cha umwagiliaji kinaendelea na matumizi mengine ya majumbani pamoja na shuleni kama anavyothibitisha Lilian Ruto Mkazi wa Kijiji cha Kapkut ambaye pia ni mkulima wa mbogamboga wa kikundi cha kina mama wa Eitui. 

“Mahali tulikuwa tunatoa maji kulikuwa mbali sana na ilikuwa inatuchukua muda ili uweze kufikisha maji nyumbani ndio uende kuendelea na kazi zako za nyumbani. Kwahiyo tunashukuru sana kwasababu maji yamefika.“ 

Bi.Ruto anasema sasa hawategemeai tena chakula cha msaada kwani wanaweza kulima wenyewe na lishe za watoto wao zimeimarika.  

“Sasa kwasababu tumepata maji tunajua sasa tuta tengeneza bustani tupande vyakula vyenye lishe ili kuhakikisha watoto wetu wanapata lishe bora.”

WFP inafanya kazi kwa karibu na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa ikiwemo UNICEF, UNEP, FAO na IFAD kuhamasisha matumizi bora ya maji kwa afya, uhakika wa upatikanaji wa chakula na ustawi bora wa maisha yao. 

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
2'19"
Photo Credit
© FAO/Fredrik Lerneryd