07 SEPTEMBA 2023
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina ambapo Magavana Dkt. Wilber Ottichilo wa Kaunti ya Vihiga na Gavana wa Kaunti ya Narok, Patrick Ole Ntutu hivi karibuni walipohudhuria Jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa kuhusu SDGs lijulikanalo kama HLPF hapa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, waliketi na Flora Nducha wa Idhaa hii ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa ili waeleze mipango yao ya kutimiza Malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu, SDGs katika majimbo yao huko nchini Kenya. Pia tunakuletea habari kwa fupi kuhusu Akili mnemba au AI, Siku ya Polisi na mkutano wa ASEAN. Katika kujifunza lugha ya kiswahili tunakuletea maana ya methali KIVULI CHA FIMBO HAKIMFICHI MTU JUA.
- Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezipongeza nchi za kusini-mashariki mwa Asia kwa mchango wake wa kujenga maelewano duniani kote wakati huu ambapo ulimwengu umegubikwa na mivutano ya kisiasa na kijiografia.
- Ikiwa leo ni siku ya Kimataifa ya Ushirikiano na Polisi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewatumia salamu za pongezi polisi ulimwenguni kote kwa kujitolea kwao kuhakikisha jamii inakuwa na amani, usalama na haki. Amewakumbusha pia upolisi unaolenga katika kusaka suluhisho za kijamii husaidia zaidi kujenga uaminifu na kuboresha usalama.
- Na tuhitimishe na masuala ya teknolojia, wakati muhula mpya wa masomo ukianza maeneo mengi duniani, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO limetoa muongozo wenye vipengele saba unaotaka nchi kudhibiti matumizi ya akili mnemba au -AI mashuleni.
- Katika kujifunza lugha ya Kiswahili Dkt Mwanahija Ali Juma, Katibu Mkuu wa Baraza la Kiswahili, Zanzibar nchini Tanzania, BAKIZA anachambua methali KIVULI CHA FIMBO HAKIMFICHI MTU JUA.
Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!