Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mama akiwa na wanae ukimbizini Chad asimulia yaliyomsibu Sudan

Mama akiwa na wanae ukimbizini Chad asimulia yaliyomsibu Sudan

Pakua

Walimuua mume wangu, walijeruhi mwanangu na mimi walinipiga, ni simulizi ya mama ambaye sasa yuko na watoto wake nchini Chad akitokea Sudan kwani nchini mwake ni kama wasemavyo wahenga, Amkani si shwari kufuatia mapigano yaliyoanza tarehe 15 mwezi Aprili mwaka huu ambayo pamoja na kuua zaidi ya watu 700 wengine zaidi ya 300,000 wamekimbilia nchi jirani ikiwemo Chad na miongoni mwao ni Hawaye Ibrahim.

Sura isiyo na matumaini na iliyopauka!!!  Hawaye Ibrahim yuko na watoto wake watatu hapa Koufroune nchini Chad kwenye kituo cha mpito cha wakimbizi kutoka Sudan, lakini mawazo hayako hapa kabisa. 

Hawaye anasema Ni mapigano yamenileta hapa. Wanamgambo waliingia nyumbani kwetu, walimuua mume wangu na wakamjeruhi mtoto wangu wa kiume .Mimi mwenyewe walinitesa, hivyo nikakimbia na kuja hapa Chad.” 

Anamnyanyua mwanae aliyejeruhiwa kuonesha kovu, anaitwa Manane, ameshonwa nyuzi 7 juu ya kitovu na 3 chini ya kitovu, angalau jeraha limepona. 

Hawaye huku sasa akionesha sikio lake anaendelea kusema, “walinipiga kwa fimbo na hadi sasa sikio langu la kushoto halifanyi kazi ,hivyo siwezi kusikia vizuri.” 

Kutoka kuishi kwenye nyumba yao huko Darfur nchini Sudan hadi kwenye kibanda hiki kilichoegeshewa na kuzungushiwa nailoni, hapa jua ni lao! na mvua ni yao. 

Akikumbuka safari yao, Hawaye anasema “nilikimbia saa tano za usiku nikiwa nimembeba mgongoni mwanangu aliyejeruhiwa. Sikuwa hata na usafiri wa punda. Ilibidi watoto wengine niwaache. Waliletwa hapa na watu wengine.” 

Hawaye akiendelea kuwaza na kuwazua akiwa na wanawe, kwingineko hapa wanawake wanaonekana wakisubiri mgao wa vifaa vya huduma za msingi huku wengine wakizidi kuwasili na virago vyao kwa kutumia punda. 

Brice Degla Mratibu Mwandamizi wa masuala ya dharura wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR nchini Chad anasema, “Wamekimbia sio tu kwa sababu ya vita mjini Khartoum, bali pia kwa sababu ya mapigano ya kikabila baina ya jamii huko Tendalti. Halikadhalika hofu ya kushambuliwa kwa sababu ya vita, imewalazimu wakimbie na ndio wote sasa wamefika hapa.” 

Katika vibanda vingine, akina mama wako na watoto wao, njaa ni dhahiri. 

Ingawa tayari kuna usalama tofauti na kule Darfur alikotoka bado Hawaye ana mahitaji akisema, “nahitaji chakula, nahitaji nguo, nahitaji pia malazi na sabuni na vitu vingine ili niweze kutulia.” 

Mgao wa bidhaa muhimu unaendelea huku wakimbizi wengine wakipanda magari wakipungiwa na wenzao waliosalia. Bwana Delga anasema , “UNCHR inabaini maeneo yaliyo mbali, angalau kilometa 50 kutoka hapa, ambako inahamishia wakimbizi kutoka hapa mpakani, ili hatari ya ukosefu wa usalama iwe imepatiwa jawabu,  lakini vile vile kuwapatia msaada.” 

Baada ya muda,  walioondoka Koufroune wamewasili Gaga nchini Chad hapa wamepatiwa angalau makazi yenye staha na sasa wanaanza maisha upya ugenini wakiwa matumaini mapigano yaliyoanza tarehe 15 Aprili nchini mwao Sudan yatamalizika ili waweze kurejea nyumbani. 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
3'18"
Photo Credit
UNHCR Video