Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO: Nchi ziache kutoa ruzuku kwa wakulima wa tumbaku

WHO: Nchi ziache kutoa ruzuku kwa wakulima wa tumbaku

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO limezisihi nchi kuacha kutoa ruzuku kwa wakulima wa tumbaku na badala yake kuelekeza usaidizi wao kwenye mazao endelevu yatakayo wanufaisha mamilioni ya watu.

Katika kuelekea sikuya kupinga matumizi ya tumbaku duniani itakayoadhimishwa Mei 31 WHO inasema  , watu milioni 300 ulimwenguni wanakabiliwa na uhaba wa chakula wakati huo huo zaidi ya hekta milioni 3 katika nchi 120 zinatumika kulima tumbaku, hata katika zile nchi zenye tatizo la njaa.

WHO katika taarifa yao kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo huko Geneva Uswisi imeeleza kuwa kwa kuchagua kulima mazao ya chakula badala ya tumbaku inamaanisha jamii inatoa kipaumbele kwenye afya, kulinda baianowai na kuimarisha uhakika wa chakula.

Akizungumzia athari za tumbaku, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema “tumbaku imesababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 8 kwa mwaka, na bado serikali duniani kote zinatumia mamilioni ya kuwasaidia wakulima wa zao hilo.”

Ripoti mpya iliyotolewa na WHO kuelekea siku ya kupinga matumizi ya tumbaku iitwayo “Lima chakula sio tumbaku” imeeleza madhara ya kulima tumbaku na faidi ambazo wakulima, jamii, uchumi, mazingira na dunia kwa ujumla itapata iwapo itahamia kwenye ukulima wa mazao mengine.

 Ripoti hiyo pia inafichua tasnia ya tumbaku kuwa inawaingiza wakulima katika changamoto mbalimbali ikiwemo mzunguko mbaya wa madeni, wakulima kupata magonjwa na watoto zaidi ya milioni 1 wametumbukia kwenye kilimo hicho na kukosa fursa ya kupata elimu.

Katika kuhakikisha wakulima wanasaidiwa kuhamia kwenye kilimo cha mazao ya chakula WHO kwa kushirikiana na mashirika mengine ya UN lile la Mpango wa chakula duniani WFP na la chakula na kilimo FAO wanawasaidia wakulima 5000 nchini Kenya na Zambia kulima mazoa ya chakula endelevu badala ya tumbaku.

Katika juhudi hizo WHO kila mwaka katika siku ya Kutotumia tumbaku huwaenzi wale wanaoleta mabadiliko chanya katika udhibiti wa tumbaku na mwaka huu mmoja wa washindi wa Tuzo hizo, Bi. Sprina Robi Chacha, mkulima wa kike kutoka nchini Kenya ambaye anatambulika si tu kwa kuachana na  kilimo cha tumbaku kuhamia kwenye maharagwe yenye protini nyingi, bali pia kutoa mafunzo kwa mamia ya wakulima wengine ili na wao waweze kutoka kwenye kilimo cha tumbaku na kujenga jamii yenye afya bora.

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
2'30"
Photo Credit
© UNICEF/Shehzad Noorani