Skip to main content

Makao Makuu ya UM: Jukwaa la 18 la Umoja wa Mataifa la misitu limeng’oa nanga leo

Makao Makuu ya UM: Jukwaa la 18 la Umoja wa Mataifa la misitu limeng’oa nanga leo

Pakua

Jukwaa la 18 la Umoja wa Mataifa la misitu limeanza leo kwenye makao Makuu ya Umoja huo mjini New York Marekani likiwaleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, mfumo wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa na kikanda na wadau wa misitu ili kujadili thamani ya rasilimali hiyo muhimu kwa binadamu na mazingira

Kwa mujibu wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO misitu ni chanzo kikubwa cha nishati, chakula na malisho, na hutoa riziki kwa mamilioni ya watu, ikiwa ni pamoja na wengi ambao ni maskini zaidi duniani.

Watu bilioni 2.4 duniani bado wanatumia nishati inayotokana na kuni kupikia. Lakini misitu pia husaidia kupunguza mabadiliko ya tabianchi na kuboresha rutuba ya udongo, hewa na maji.

Shirika hilo linasema ikisimamiwa kwa uendelevu, misitu pia ni chanzo cha malighafi inayoweza kurejelewa, na hivyo kutoa mchango muhimu katika mzunguko wa ujenzi wa uchumi.

Jukwaa hili lililoandaliwa na idara ya masuala ya kiuchumi na kijamii ya Umoja wa Mataidfa DESA linataka kila mtu duniani afahamu mambo matano muhimu kuhusu misitu ambayo ni mosi misitu inachukua asilimia 31 ya eneo la dunia,ina asilimia 80 ya bayoanuai ya dunia na inahifadhi hewa ukaa kiasi kikubwa zaidi ya kilichopo hewani.

Pili, misitu inasaidia ustawi na maisha ya viumbe duniani, kwani watu zaidi ya bilioni 1.6 wanategemea mistu ili kuishi, kuendesha Maisha yao, ajira na kipato na Afrika takriban watu bilioni 2 na kaya theluthi mbili bado wanategemea misitu kwa kuni kama nishati ya kupikia

Tatu misitu yenye afya inasaidia afya ya watu kwani misitu na miti inatoa hewa safi na maji na maji ni Uhai bila kujali mtu anakoishi.

Nne misitu inaendelea kuwa hatarini kila mwaka dunia inapoteza ekati milioni 10 za misitu sababu ya uktaji haramu wa magogo, moto wa nyika, uchafuzi wa mazingira, magonjwa, wadudu na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Na tano kurejesha misitu ni ufunguo wa kuwa na mustakbali endelevu na kurejesha ardhi iliyomomonyoka kutasaidia kufikia malengo ya maendeleo endelevu hasa ya kuongeza eneo la mistu duniani kwa asilimia 3 ifikapo mwaka 2030.

Kongamano hilo la siku 5 litakunja jamvi Ijumaa Mei 12

Audio Credit
Flora Nducha
Sauti
2'32"
Photo Credit
UNEP/Lisa Murray