Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajumbe wa Baraza la Usalama watamatisha ziara DRC

Wajumbe wa Baraza la Usalama watamatisha ziara DRC

Pakua

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wametamatisha ziara yao ya siku tatu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC iliyolenga kujadili kwa kina majukumu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO halikadhalika kujionea hali halisi ya amani na usalama.

Kupitia mtandao wa Twitter, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa nchini DRC, Bintou Keita amesema wajumbe wa Baraza pamoja na kuwa na mazungumzo na viongozi wa ngazi ya juu wa serikali na MONUSCO,  walipata pia fursa ya kutembelea maeneo ya Mashariki wa taifa hilo ambako kumegubikwa na mashambulizi kutoka makundi ya waasi. 

Mathalani walipata fursa ya kusikiliza shuhuda kutoka kwa wawakilishi wa vikundi vya wanawake jimboni Kivu Kaskazini, vikundi ambavyo vinapambania kuheshimiwa kwa haki za wanawake na wasichana waliokumbwa na ukatili wa kingono. 

Halikadhalika walitembelea kambi ya wakimbizi ya ndani ya Bushagara – Nyiragongo ambako iko karibu na Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.

Bi. Bintou ambaye pia ni Mkuu wa MONUSCO amesema katika kambi hiyo maelfu ya wakimbizi wa ndani wako hatarini na mazingira yao yanakabiliwa na changamoto lukuki. 

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ina takribani wakimbiz iwa ndani milioni 5 na mashambulizi kutoka makundi ya waasi yanazidi kukwamisha maisha yao.

Audio Credit
Flora Nducha
Sauti
1'22"
Photo Credit
MONUSCO