Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jamii Somaliland zasaidiwa kupambana na uhaba wa chakula: FAO

Jamii Somaliland zasaidiwa kupambana na uhaba wa chakula: FAO

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO linaendesha mradi wa miaka minne wa mnepo wa uhakika wa upatikanaji wa chakula katika maeneo yaliyoathirika na migogoro pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi katika pembe ya Afrika lengo likiwa ni kujenga amani na kutatua changamoto wanazo kabiliana nazo.

Video ya FAO ikimuonesha Asha Mohammed Ali mama wa watoto 8 na mkulima kutoka wilaya ya Wadaamago huko Somaliland akiwa shambani anapalilia mazao yake huku akisimulia namna ukame ulivyowaathiri wakulima na kuharibu kabisa mustakabali wa maisha yao.

Anasema “Mifugo imeathiriwa na ukame na kilimo kimeathiriwa na ukame na hata sisi wenyewe tumeathiriwa sana na ukame”

Ili kutatua changamoto zote hizo, FAO inaendesha mradi wa miaka minne kwa ufadhili wa fedha kutoka Uholanzi ambapo wanasaidia kaya 13,000 zilizoko Sool na Sanaang huko Somaliland kwa kuwapatia malisho ya mifugo yao, usaidizi kwenye kilimo pamoja na mbinu bora za kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi.

“Kupitia mradi huu katika eneo letu, tulipewa mafunzo ya kuzalisha mazao na matunda, na pia tulikuwa tunapewa trekta kwa saa kadhaa, walituletea mashine za lishe na vifaa vingine na kutujengea kituo cha kuhifadhi mazao. Tulipatiwa ujuzi wa kufanyakazi, kuongeza juhudi, tumefundishwa kuungana na kushirikiana yani tufanye kazi pamoja. Kwakweli tumejifunza mengi kutoka FAO.”

Juhudi kama hizi zinawasaidia watu kama Asha kuweza kuendesha maisha yao hata kama wanakabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
1'45"
Photo Credit
FAO