Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen: Badala ya kununua sabuni sasa nanunua chakula, asante UNICEF

Yemen: Badala ya kununua sabuni sasa nanunua chakula, asante UNICEF

Pakua

Huduma za kujisafi na usafi mara nyingi husalia ndoto kwa wakimbizi wa ndani kwa kuwa kipaumbele kinakuwa ni usalama wao hali inayoongeza zaidi hatari ya kupata magonjwa iwapo wanakosa huduma hizo na ndio maana nchini Yemen, Umoja wa Mataifa umechukua hatua kuwezesha wayemen waishio kambini wanaweza kujikinga pia na magonjwa yatonayo na uchafu.

Ndivyo ianzavyo video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF ni Saeedah Ahmed Mohammed Mohinish akijtambulisha, akisema kuwa hafahamu umri wake, na zaidi ya yote hajui kusoma na kuandika. Ana watoto 10, watano ni wavulana na watano wasichana. 

Saeedah yuko kwenye kibanda chake hapa kambini al Alili wilaya ya Al Khawkhah jimboni Hudaydah nchini Yemen. Aliwasili hapa miaka minne iliyopita, “Nilikuja hapa na familia yangu. Maisha hapa ni magumu lakini tumezoea. Tulipata mgao wa vikasha vya kujisafi, zikiwemo sabuni na madumu ya kuhifadhi maji. Tulielimishwa pia kuhusu umuhimu wa usafi binafsi kama vile kufua nguo na kunawa mikono kwa usahihi.” 

Mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa UNICEF unaotekelezwa na Taasisi ya Taybah na kufadhiliwa na shirika la Marekani la misaada kwa maendeleo ya kimataifa, USAID uliolenga watu 300,00 akiwemo Saeedah. 

Walipatiwa pia sabuni ya kufua nguo, dumu la kutumia chooni na beseni la kufulia nguo. 

Na sasa Saeedah anaona mabadiliko akisema, “Vifaa hivi vinasaidia kuimarisha sana usafi wetu. Tunafua nguo na tunaoga. Wakati mwingine tulitumia dola 1 na senti 20 kununua sabuni, lakini sasa tunatumia fedha hizo kununua mboga za majani na vyakula vyenye lishe.tunashukuru UNICEF na washirika wake kwa kutupatia vifaa hivi.” 

Ili kusongesha usafi kwenye kaya, UNICEF inafundisha walezi juu ya umuhimu wa kunawa mikono kabla ya kula chakula, kabla ya kumlisha mtoto, kabla ya kupika na baada ya kumbadilisha nepi mtoto. 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'20"
Photo Credit
© UNICEF/SalehHayyan