Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN: Wanaume na wavulana jitokezeni mtokomeze FGM

UN: Wanaume na wavulana jitokezeni mtokomeze FGM

Pakua

Hii leo ni ikiwa ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji wa wanawake na wasichana ,Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka wanaume na wavulana wapaze sauti zao kusaidia kutokomeza mila hiyo potofu na hatarishi.  

Ujumbe wa siku hii kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia Watoto, UNICEF na lile la afya ya uzazi na idadi ya watu duniani, UNFPA ni “Nafasi ya ubia na wanaume na wavulana katika kurekebisha maadili ya kijamii na kijinsia ili kutokomeza FGM.”  

Na ndio maana katika ujumbe wake Katibu Mkuu ametanabaisha kuwa FGM imejikita katika ukosefu wa usawa kijinsia na maadili ya kijamii yanayokwamisha ushiriki wa wanawake katika uongozi, na kuwabana fursa yao ya elimu na ajira. 

Guterres amesema ubaguzi wa aina hii unaharibu jamii nzima na inahitajika hatua ya dharura ya jamii nzima kutokomeza. 

Katibu Mkuu amesema, “wanaume, wavulana — kaka, baba, wahudumu wa afya, walimu na waganga wa jadi wanaweza kuwa washirika thabiti katika kuhoji na kutokomeza janga hili, kama ambavyo maudhui ya mwaka huu yanadhihirisha. Natoa wito kwa wanaume na wavulana kokote waliko waungane nami katika kupaza sauti na kujitokeza kuondoa FGM kwa maslahi ya wote.” 

Amesisitiza kuwa ukeketaji wanawake na watoto wa kike ni ukiukaji wa haki za msingi za kibinadamu unaoleta madhara ya kimwili na kiakili maisha yote ya yule aliyefanyiwa n ani moja ya vitendo vinavyosongesha mfumo dume uliojikita duniani. 

Takwimu zinaonesha kuwa takribani Watoto wa kike milioni 4.2 duniani wako hatarini kukeketwa mwaka huu wa 2023 pekee. 

Ni kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametaka uwekezaji wa dharura na hatua thabiti ili kufikia lengo la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs la kutokomeza kitendo hicho ifikapo mwaka 2030. 

Guterres ametamatisha ujumbe wake akitaka siku ya leo itumike kwa kila mtu kuahidi kuleta mabadiliko ya kijamii na kujenga ubia thabiti wa kutokomeza FGM sasa na wakati wote. 

Akizungumza katika mikutano mbalimbali ya ngazi ya juu hii leo mjini Dublin Ireland ikihusisha wawakilishi wa serikali na wadau wengine wa kimataifa wa elimu Yasmine Sherif mkurugenzi wa Education Cannot Wait, ECW au elimu haiwezi kusubiri amesema “Hivi sasa watoto na barubaru milioni 222 walio katika maeneo ayliyoathirika na migogoro wanahitaji haraka msaada wa elimu na zaidi ya nusu yao ni wasichana. Ni muhimu sana mfuko wa elimu haiwezi kusubiri kufandiliwa kikamilifu ili kuhakikisha wadau wetu wa kimataifa kama Plan International wanaweza kuendelea na kazi yao nyeti ya kutoa usalama, matumaini na fursa za elimu kwa wasichana na wavula walio katika hali mbaya zaidi duniani.” 

Bi. Sherif amesema ufadhili huo wa elimu uitasaidia kutimiza malengo ya ajenda ya mwaka 2030 ya maendeleo endelevu ikiwemo ahadi ya elimu kwa wote. 

Mkurugenzi Mtendaji wa kimataifa wa Plan International Stephen Omollo, aliyeambatana na Bi. Sherif katika mikutano hiyo ameongezea kuwa
“Kwenda shule ni njia ya ukombozi wa maisha kwa watoto, hasa wasichana. Hata hivyo, duniani kote, watoto wananyimwa haki hii ya msingi. Tumesikia kuhusu kukaribia kupigwa marufuku kwa elimu ya wasichana nchini Afghanistan na matokeo mabaya ya hili. Lakini kunyimwa haki ya msingi ya elimu kwa wasichana kunakwenda mbali zaidi ya Afghanistan. Kuanzia Ukraine hadi Sudan Kusini, migogoro inavuruga elimu ya wasichana huku familia zikilazimika kukimbilia usalama wao na hakika, nusu ya watoto wote wakimbizi hawako shuleni, nahii si haki.” 

Ameendelea kusema kuwa katika nchi nyingi elimu imekatizwa kutokana na njaa au mabadiliko ya tabianchi au wakati mwingine mchanganyiko wa mjanga yote hayo, “Na wasichana wanapolazimika kuacha shule sio tu elimu yao na fursa zao zinazoathirika hususan kwa wasichana vigori wanakuwa katika hatari ya ukatili, manyanyaso, mimba za utotoni na mila zingine potofu za kikatili  kuanzia ndoa za utotoni hadi ukeketaji. "

Wadau hao wa elimu wameeleza kuwa migogoro, mabadiuliko ya tabianchi na majanga mengine vimeongeza mara tatu idadi ya watoto na vijana barubaru wanaohitaji msaada wa elimu kutoka milioni 75 mwaka 2015 hadi kufimia milioni 222 mwaka huu. 

Kwa mantiki hiyo wamesisitiza haja ya jumuiya ya kimataifa ikiwemo Ireland kusaidia kufadhili mfumo huo wa elimu haiwezi kusubiri kwenye mkutano wa ufadhili wa elimu haiwezi kusubiri utakaofanyika Geneva Uswis mwaka huu kuanzi Februari 16-17. 

Audio Credit
Thelma Mwadzaya
Audio Duration
2'10"
Photo Credit
UNICEF/Furrer