Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchini Sierra Leone, IFAD yawasaidia wanawake wenye ulemavu kuondokana na umaskini

Nchini Sierra Leone, IFAD yawasaidia wanawake wenye ulemavu kuondokana na umaskini

Watu wenye ulemavu wanaeleza kakabiliwa na ubaguzi mkubwa huko vijijini nchini Sierra Leone, na wakiwa mwanamke ndio kunafanya mambo kuwa mabaya zaidi, huku wengi wakishindwa kupata kazi.

Kwa kutambua umuhimu wao katika jamii , Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya kilimo duniani, IFAD imefanya jambo ili kuwaondoa wanawake hawa katika umasikini. Ni jambo gani hilo?

Katika eneo la Kabala lililoko Kaskazini mwa nchi ya Sierra Leone hali ni ngumu kwa wanawake wenye ulemavu kupata kazi za kujipatia kipato. Mariama Jalloh mkulima mwenye ulemavu anasema “Wanawake wenye ulemavu wanakabiliwa na ubaguzi kwa kiasi kikubwa na matatizo mengine mengi katika jamii.”

Kutokana na hali hiyo alianzisha ushirika ambao unafanya jukumu la kuwatetea na kuwasaidia wenye ulemavu kukabiliana na vikwazo vingi wanavyokutana navyo pamoja na kuwapatia ajira.

Kabla ya janga la COVID-19 wanachama wa ushirika huo walikuwa wakijishughulisha na ushonaji na kutengeneza sabuni na kama ilivyo kwa mamilioni ya watu duniani nao waliathirika kwa kiasi kikubwa.

“Kadri mfumuko wa bei ulivyokuwa ukiongozeka nasi tulikuwa tunapoteza wateja wetu wengi sababu watu walikuwa wanatumia hela zao kununua chakula badala na bidhaa zetu tunazotengeneza. Maisha hayakuwa rahisi kwetu, kwasababu tulishindwa kuzihudumia familia zetu.

Changamoto hii ikawafanya wahamie katika kilimo lakini kutokana na ulemavu wakatakiwa kuajiri watu wa kuwasiadia kulima na hapa ndipo Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya kilimo duniani, IFAD ukaja kuwa msaada kwa ushirika huo kwani uliwapatia fedha za kuweza kukabiliana na changamoto za COVID-19, fedha za kuajiri wafanyakazi shambani, mbegu  na zana nyingine za kilimo ili waweze kutimiza lengo lao.

“Kama wasingekuja na kutusaidia, tusingeweza kufanikiwa katika lengo letu.”

Ufadhili huu wa IFAD uliweza kuokoa maisha ya wengi kwani uliwawezesha kujikimu wao na familia zao.

 

Pakua
Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Audio Duration
2'9"
Photo Credit
IFAD Video