Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mada kwa kina: Chanjo dhidi ya Kipindupindu yaendelea Kivu Kaskazini, DRC

Mada kwa kina: Chanjo dhidi ya Kipindupindu yaendelea Kivu Kaskazini, DRC

Pakua

Kampeni ya utoaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu  iliyoanza tarehe 25 mwezi huu huko Kivu Kaskazini nchini jamhuri ya Kidemokraia ya Congo, DRC imekunja jamvi jana Jumanne ya tarehe 30 mwezi hu uwa Januari ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO lilizindua kampeni hiyo ya chanjo kwa wakimbizi wa ndani katika kambi ya wakimbizi hao ya Kanyaruchinya wilayani nyiragongo katika mji wa Goma jimboni Kivu Kaskazini.

Mwandishi wetu wa DRC Byobe Malenga ambaye ameshuhudia uzinduzi huo amesema uliongozwa na Gavana wa jimbo la Kivu Kaskazini Jenerali Ndima Constant, na Mwakilishi wa shirika WHO nchini DRC kwa lengo la kuokoa mamia ya familia hususan za wakimbizi wa ndani ambao tayari makumi kwa makumi wameripotiwa kupata ugonjwa huo na wengine wamefariki dunia.

Jean Bruno, ni Mkuu wa Ofisi ya WHO Kivu Kaskazini na anasema ameridhishwa na shauku ya siku ya kwanza na zaidi ya yote amesema,

« Tumewalenga watu 364,127 ambao ni wakimbizi wa ndani, pamoja na familia zinazowapokea. Tayari tumepokea dozi 364,150 ambazo zipo na zitatumika. chanjo itafanyika kwa awamu ya dozi moja na tutafanya hivyo kupitia kampeni ya nyumba kwa nyumba kwenye maeneo haya . Tumeridhika na ukweli ni kwamba kumekuwa na dhamira muhimu kwa upande wa serikali kwenye ngazi ya taifa na mkoa, lakini pia tumekuwa na hakikisho kutoka kwa jamii ya watu na wakimbizi wa ndani ambayo imekubali chanjo hiyo ambayo itafanyika kwa wakati».

Eneo la Nyiragongo lilipokea idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na mashambulizi yanayofanywa na waaasi wa M23 huku watu 233 elfu waliokimbia makazi yao, zaidi ya 95% yao wamelundikana kwenye makanisa, shule, viwanja vya michezo na maeneo yasio salama kwa afya yao.

Gavana wa Kivu Kaskazini, Jenerali Ndima Constant, anakiri kwamba janga la kipindupindu linaathiri sana eneo la Nyiragongo akisema kwamba hadi Jumanne ya Januari 24  wagonjwa 3706 wa kipindupindu walisajiliwa huku kukiwa na vifo 16 na ili kupunguza mlolongo wa maambukizi amewasihi raia kupata chanjo akishukuru WHO kwa msaada wao.


« Madhumuni ya kampeni hii  ya chanjo ni kulinda idadi ya watu dhidi ya kipindupindu katika jimbo la Kivu Kaskazini na hasa katika maeneo ya watu waliofurushwa ili kupunguza vifo. Mabibi na mabwana, wageni mashuhuri, ili kufunga maoni yangu, ningependa kuwakumbusha kuwa pamoja na chanjo utakayopokea, kufuata hatua za kuzuia maambukizi ni muhimu..”

Ametaja njia za kujikunga kuwa ni pamoja na kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi na sabuni au majivu, kunywa maji yaliyotakasishwa tu au yaliyochemshwa. Kupika na kufunika milo yetu, matumizi sahihi ya vyoo huku tukiwa wasafi na kuweka usafi kwenye maeneo yetu ya makazi  kila wakati.

Waliokimbia makazi yao wanafahamu tishio hilo kwa sababu janga hilo limeathiri zaidi ya 89% ya waliokimbia makazi katika miezi ya hivi karibuni na chanjo inatekelezwa nyumba kwa nyumba.

Watu waliohamishwa wanasubiri dozi zao nyumbani. Damaseni Butera ni miongoni mwa watu wa kwanza kupata dozi moja dhidi ya kipindupindu na anashukuru mpango huu wa WHO na anasema, «chanjo ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya magonjwa kama kipindupindu, malaria na mengine.Tumejifunza habari kuhusu chanjo hiyo, tumefurahi sana kwa sababu tutakuwa na kinga, asante sana kwa shirika la WHO ambalo lilitufikiria. Asante sana»

Kando na hilo, Mweze Shemba, aliyekimbia kutoka kijiji cha Kiwanja, pia alinufaika na chanjo hii. Licha ya njaa,yeye anapendelea kujilinda pamoja na familia yake dhidi ya janga hili akisema, «kilichonifanya nipate chanjo ya leo hapa katika kambi ya wakimbizi ni kwa sababu tunapatwa na magonjwa ya taabu. kama vile kuhara na kutapika hasa tunapokunywa maji machafu. Lakini wakati tunapata hii chanjo tunaona kama vile ni kinga kwetu tunashukuru sana »

Katika juhudi za kuepusha msongamano wa wagonjwa wa janga hili , WHO ilijenga vitalu 3 kama kitengo cha matibabu ya wagonjwa wa Kipindupindu (UTC) katika eneo la Bushagara na Nyiragongo. chini ya usimamizi wa shirika la MEDAIR.

Audio Credit
Byobe Malenga
Audio Duration
5'30"
Photo Credit
UN News/ Byobe Malenga.