Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO limesema magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika mbioni kutokomezwa duniani

WHO limesema magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika mbioni kutokomezwa duniani

Pakua

Shirika la Umoja wa MAtaifa la afya ulimwenguni, WHO, limesema mataifa mengi zaidi duniani yametokomeza magonywa ya kitropiki yaliyosahaulika, au NTDs huku ikisema bado uwekezaji zaidi unahitajika kusongesha maendeleo hayo dhidi ya magonjwa hayo kama vile ukoma, vikope na kung’atwa na nyoka.

Kauli hiyo ya WHO imetolewa leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kuhamasisha dhidi ya magonjwa hayo ya kitropiki yaliyosahaulika, NTDs na shirika limeweka hayo bayana kwenye ripoti mpya iitwayo Ripoti ya Dunia kuhusu NTDs kwa mwaka 2023.

 

Ripoti imetaja mafanikio na changamoto ya kutibu NTDs duniani kote wakati huu ambapo matibabu yalivurugwa na mlipuko wa COVID-19.

 

Mafanikio ni pamoja na idadi ya wagonjwa kupungua kwa milioni 80 kati ya mwaka 2020 na 2021 huku nchi 8 zikithibitishwa kutokomeza moja ya magonjwa hayo mwaka 2022 pekee na kufanya idadi ya nchi zisokuwa na NTDs duniani kote hadi mwezi Desemba mwaka jana kufikia 47.

Hata hivyo ripoti inasisitiza uwekezaji zaidi kuchagiza kasi ya kutokomeza magonjwa hayo yanayoathiri maskini zaidi ili kufikia malengo ifikapo mwaka 2030.

Mathalani uwekezaji unaopatia uwezo taifa kumiliki na kuwajibika na tiba na ufadhili wa  uhakika.

NTDs inaathiri zaidi jamii maskini hasa kwenye maeneo ambako huduma za maji safi na kujisafi ni haba, halikadhalika huduma za afya.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akizungumzia ripoti hiyo amesema duniani kote mamilioni ya watu wamekombolowe kutoka katika mzigo wa magonjwa hayo ambayo yanawatumbukiza kwenye mzunguko wa umaskini na unyanyapaa.

Amesema “ingawa kuna hatua zaidi zinahitajika, lakini habari njema ni kwamba tuna mbinu na ufahamu wa sio tu kuokoa maisha na kuzuia machungu, bali pia kuokoa jamii nzima na mataifa yote dhidi ya ugonjwa huu. Wakati wa kuchukua hatua ni sasa, tuwekeze kwenye NTDs.”

Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
2'3"
Photo Credit
© UNICEF/Olivier Asselin