Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya: Mradi wa Teen Seed Africa warejesha matumaini ya elimu kwa wasichana waliopata mimba za utotoni

Kenya: Mradi wa Teen Seed Africa warejesha matumaini ya elimu kwa wasichana waliopata mimba za utotoni

Pakua

Umoja wa mataifa kwa ushirikiano na serikali ya Kenya ulizindua mwaka 2015 mradi wa kuwarejesha watoto shule walioacha kwa sababu moja au nyengine. 

Kupitia mashirika mbalimbali kama Educate A Child, Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na lile la idadi ya watu duniani UNFPA ilizindua miradi ya pamoja ya kuwarejesha watoto shule. 

Utafiti wa hivi karibuni  wa mashirika hayo umebainisha kuwa moja ya chanzo kikuu cha watoto wa kike kuacha shule ni mimba za utotoni na hususan watoto ambao wanaishi katika mitaa ya mabanda.  

Maisha katika mitaa ya mabanda yana changamoto za kila aina ikiwmo usalama mdogo, msongamano, na uhaba wa huduma za kijamii ambavyo vyote vinachangia kuwapa changamoto kubwa wasichana. 

Kwa mujibu wa UNFPA, kila siku, wasichana alfu 20 walio na umri ulio chini ya miaka 18 hujifungua. Hii ni sawa na watoto milioni 7.3 kwa mwaka kote duniani. 

Miongoni mwa idadi hiyo asilimia kubwa ya wasichana hujikuta wakipata ujauzito katika umro mdogo na pindi msichana anapopata uja uzito basi maisha yake hubadilika kwa kiasi kikubwa. 

Mimba za utotoni hupindua maisha ya mtoto wa kike kwani uwezekano wa kuacha shule au kurejea baada ya kujifungua kwa kiasi kikubwa ni mdogo sana.Mara nyingi chanzo cha mimba za utotoni ni ukosefu wa elimu au kusoma shuleni, taarifa na hata huduma mujarab za afya.  

Hali hiyo ndiyo iliyolisukuma shirika la kijamii la Teen Seed lililoko mtaa wa mabanda wa Kiambio kuzindua mradi wa kuwarejesha shule wasichana waliopata mimba utotoni. Zawadi Anthony ni mratibu wa mradi wa Teen Seed Africa na anaelezea kuwa,”Wanapokuja wasichana tunakagua na kubaini iwapo wanataka na wana uwezo wa kurejea shule.Kisha tunahakikisha kuwa wanapata kila wanachohitaji ima ni vifaa vya shule, mlezi wa watoto au mtoto,bidhaa za matumizi na vyote anavyohitaji kukamilisha masomo yake.Kwa kawaida tunamtafutia shule hapa hapa karibu mtaani tu.”anafafanua. 

Kulingana na utafiti wa mwaka 2021 wa tathmini ya watoto wasioenda shule uliofanya na mradi wa OOSC wa Educate A Child unayoshirikiana na UNICEF, watoto wasioenda shule walio na umri wa kati ya miaka 6 hadi 13 ni milioni 1.13 na wanazurura mitaani. 

Ripoti iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu , sayansi na utamaduni UNESCO mwaka jana kuhusu changamoto za elimu inasema changamoto na vikwazo vya janga la COVID 19 vimesababisha na vinaendelea kuwaathiri wazazi wengi hasa katika nchini zinazoendelea kukimu mahitaji ya familia zao. Hii imechangia kwa baadhi ya watoto wa kike kujikuta pabaya na kuingilia mambo yasiyofaa kupata mkate wa kila siku. Quinta Faith ni msimamizi wa kitengo cha wasichana katika shirika la Teen Seed Africa na anaelezea wanachokumbana nacho ni,Wasichana huamua kuolewa mapema wakiwa na miaka 14 au 16 kwani wamekosa wa kumtegemea kutimiza mahitaji yao ya kila siku.Umasikini ndio unaowasukuma kuwaegemea wanaume ambao wamewaonyesha mapenzi.anasimulia. 

Kwa ushirikiano na shirika la kijamii la Educate a Child, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF, linafanya kazi pamoja na serikali ya Kenya kuiongeza idadi ya watoto wanaorejea shuleni baada ya kuacha shule kwa sababu moja au nyingine. 

Mimba za utotoni ni moja ya sababu kuu za watoto wa kike kuacha masomo. Na mimba hizo zinaweza kutokea katika mazingira mbalimbali ikiwemo kwa na kuaacha wakiwa wamechanganiyikiwa.  

Hapo ndipo Sharon Adema mshauri nasaha katika shirika la Teen Seed Africa anawapokea na kuwashika mkono na kwanza,” Tunawapokea wakiwa hali mbaya na ni dhahiri wamedhulumiwa kwani baadhi wana alama mwilini.Wakiridhia tunawapa ushauri nasaha na pia kuwapeleka hospitali kwa matibabu.Baada ya hapo tunashirikiana na afisi ya watoto ya serikali watakaoamua iwapo anaweza kurejea kwenye mazingira aliyokuwa au asalie mikonini mwao.Dhamira ni kuwaondoa kwenye mazingira magumu na hatari,” anasisitiza. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la UNFPA, liko mstari wa mbele pia kuunga mkono juhudi za kuwarejesha watoto shule ili wapate nuru ya maisha ya siku za usoni. 

Wasichana wanaoridhia kurejea shule wanapata mafunzo ya ujuzi wa kukimu mahitaji ya kila siku kutoka kwa shirika hilo kama vile kusuka mikeka, kufanya biashara na hata kupiga picha kuelezea yaliyowasibu.  

Tony Otieno ni mwelekezi wa masomo ya kupiga picha na anaelezea ya muhimu katika fani hiyo nayo ni,” Muhimu kabisa ni kuelezea kinachomsibu kwa kufuata kanuni za moja kwa moja za kupiga picha.Tunawafunza kuhusu matumizi ya kamera na pia njia mujarab ya kupiga picha ukizingatia mwanga uliopo na mada anayokusudia kuwasilisha.”anaelezea. 

Miradi kama hii inayoungwa mkono na Umoja wa mataifa kupitia UNICEF NA UNFPA imeleta tija katika maisha ya wasichana waliojikuta nje ya mazingira ya shule.  

Takwimu za UNFPA zinaashiria kuwa takriban wasichana alfu 330 hupata mimba za utotoni kila mwaka na asilimia kubwa wanatokea mitaa ya mabanda kama Kiambio.

Audio Credit
Thelma Mwadzaya
Sauti
6'41"
Photo Credit
UN News Video/Thelma Mwadzaya