Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waliofungwa kwa kusimamia haki zao waachiliwe huru- Türk

Waliofungwa kwa kusimamia haki zao waachiliwe huru- Türk

Pakua

Kufuatia kuanza kwa maadhimisho ya miaka 75 tangu kupitishwa kwa Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, UDHR, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu, Volker Türk ametoa wito kwa serikali duniani kote na mamlaka zote zinazoshikilia watuhumiwa kuwapatia msamaha au kuwaachilia huru wale wote walioswekwa ndani kwa kutekeleza haki zao za msingi.

Katika taarifa yake iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu mjini Geneva, Uswisi hii leo, Bwana Türk ametaja watu hao kuwa ni wale wanaofanya kazi kutetea na kulinda mazingira, hatua kwa tabianchi, wanaokemea ubaguzi, ufisadi, wanahabari waliofungwa kwa kutekeleza jukumu lao adhimu na watetezi wa haki za binadamu.

Kamishna huyo amesema tamko lake hili la leo linazingatia hisia alizopata akianza mwaka mpya yeye na familia yake huku akifikiria familia ambazo wapendwa wao wanashikiliwa korokoroni au wamefungwa jela kwa kutetea au kusimamia haki zao.

Ni kwa mantiki hiyo anasema, “tunapoanza maadhimisho ya miaka 75 ya Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, natoa wito kwa serikali na mamlaka zote zinazoshikilia watuhumiwa duniani kote zipatie msamaha au ziwaachilie huru wale wote wanaoshikiliwa kwa kutekeleza haki zao.”

Amezitaka mamlaka hizo zifanye hivyo kwa kupitia upya kesi dhidi ya watu hao na zichague kuanza mwaka huu wa 2023 kwa hatua ya mwelekeo wa dira ya tamko la Umoja wa Mataifa la haki za binadamu, la kuwa na dunia ambamo kwayo kila mtu anaishi huru, kwa utu na kwa haki.

Ametoa wito kwa wale walio madarakani kutekeleza tamko hilo kwa vitendo na waachene kabisa na tabia ya kukamata watu kiholela na kuwasweka korokoroni.

Tamko la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa lilipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1948.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
1'55"
Photo Credit
EQUIS Justicia para las mujeres/Scopio