Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana 'wafuma' amani wajengewe uwezo ili kulinda maliasili kwenye jamii zao

Vijana 'wafuma' amani wajengewe uwezo ili kulinda maliasili kwenye jamii zao

Pakua

Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabili madawa ya kulevya na uhalifu, UNODC, Ghada Waly amesema pamoja na kufanya tafiti za kuelewa vema uhusiano kati ya uhalifu wa kupangwa na ugaidi barani Afrika, ni muhimu pia kuwa na sera na miradi ya kukabili vitendo hivyo haramu. Taarifa ya Ibrahim Rojala wa Televisheni washirika Mamlaka TV kutoka Tanzania inafafanua zaidi. 

Bi. Waly amesema hayo wakati akihutubia kwa njia ya video mjadala wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu amani na usalama barani Afrika, hususan kuimarisha mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa maliasili ambao hufadhili makundi yaliyojihami na magaidi.

Na ndipo Idhaa ya Umoja wa Mataifa ikataka ufafanuzi zaidi kufahamu iwapo UNODC inashirikisha jamii kwenye miradi kama njia ya kukabili usafirishaji haramu wa maliasili ambapo Bi. Waly akataja vijana!

“Asilimia 60 ya watu wengi barani Afrika wana umri wa chini ya miaka 25. Vijana ndio mustakabali wa bara hili na pia ndio wako hatarini zaidi. Lakini tunafahamu pia kuwa wakiwezeshwa, vijana hawa hawa ni waleta mabadiliko, wanaweza kujenga mustakabali bora, na kuchechemua kwa niaba yao, na kwa niaba ya jamii yao na pia kulinda maliasili.”

Akatolea mfano moja ya mradi wanaotekeleza kwa pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni kupitia mfuko wa ujenzi wa amani ,

“Tunajengea uwezo vijana kuwa wajenzi wa amani kwenye maeneo ya mipakani ya Gabon, Cameroon na Chad. Lengo la mradi huu ni kujenga mtandao wa vijana 1800 wajenzi wa amani, ili hatimaye wawe watendaji katika kuzuia mizozo, ujenzi wa amani kwenye maeneo ya mpakani, na kuwawezesha kuibua mbinu mbadala za kujipatia kipato kwa jamii za mipakani.”

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa UNODC, biashara haramu ya pembe za ndovu pekee huzalisha kipato haramu cha dola milioni 400 kila mwaka.

Afrika ikiwa na idadi ya watu takribani bilioni 1.3, kati yao milioni 500 mwaka jana waliishi kwenye ufukara na kwamba biashara hiyo haramu inapora Afrika mapato, sambamba na watu wanaotegema maliasili hizo fursa ya kujipatia kipato, na wakati huo huo huchochea mizozo na ukosefu wa utulivu.

Audio Credit
Assumpta Massoi/Ibrahim Rojala
Sauti
2'11"
Photo Credit
© UNODC/Piotr Zarovski