Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walimu wasio na sifa ni moja ya sababu za janga la elimu duniani- UNICEF

Walimu wasio na sifa ni moja ya sababu za janga la elimu duniani- UNICEF

Pakua

Mkutano wa Ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu marekebisho ya mfumo wa elimu duniani ukianza leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF limetoa taarifa inayoeleza idadi ya Watoto wasiojua kusoma imeongezeka ulimwenguni ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita.Tupate taarifa zaidi kutoka kwa Assumpta Massoi

Jijini New York, Marekani katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, UNICEF wameweka mfano wa darasa kando mwa bustani ya mawaridi, darasa hili linaitwa “Darasa la Mgogoro wa kujifunza”, lengo ni kufikisha ujumbe wa changamoto ya elimu duniani hivi sasa. 
Katika kuhakikisha wanafikisha ujumbe wa changamoto ya elimu UNICEF wameweka mfano wa darasa kando mwa bustani ya mawaridi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, darasa hili linaitwa “Darasa la Mgogoro wa kujifunza”.
Darasa hili limewekwa ubao na madawati lakini theluthi moja ya madawati hayo yametengenezwa kwa mbao na kuwekwa mabegi ya mgongoni ikiwakilisha theluthi moja ya Watoto wenye umri wa miaka 10 wanaokadiriwa kuwa na uwezo wa kusoma na kuelewa ulimwenguni.
Kabla ya Janga la COVID-19 miaka miwili iliyopita watoto waliojua kusoma wenye umri wa miaka 10 ulimwenguni walikuwa nusu lakini sasa UNICEF linasema idadi yao ni theluthi moja hii ikiwa sawa na mtoto mmoja kati ya watatu ndio mwenye uwezo wa kusoma na kuelewa hadithi fupi.
Katika taarifa yake iliyotolewa jijini New York Marekani Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell ameeleza sababu za kuporomoka kwa uwezo wa Watoto kujua kusoma ni shule zilifungwa muda mrefu kipindi cha janga la CORONA na kuwaacha mamilioni ya Watoto bila ujuzi wa msingi wa kusoma na kuhesabu, elimu haikuwa bora na kufichua mapungufu mengi ndio maana idadi ya Watoto wasiojua kusoma na kuhesabu imeongezeka kwa kiwango cha kushtusha na kuonya hii ni hatari kwa Maisha ya baadae ya watu wote duniani.
Taarifa hiyo imemnukuu Bi Russelle akisema “Mifumo yetu ya elimu ndio mwelekeo wa maisha yetu ya baadae. Tunahitaji kubadili mwelekeo wa sasa au itatubidi kukabiliana na matokeo ya kushindwa kuelimisha
kizazi chote. Viwango vya chini vya kujifunza vya leo inamaanisha fursa ndogo kesho.”
Wakati viongozi wakikutana katika Mkutano wa marekebisho ya mfumo wa elimu UNICEF imetoa wito kwa serikali kujitolea kuwafikisha Watoto elimu bora kwa kuongeza uwekezaji kwenye elimu, kuweka mazingira salama ya kujifunzia, kuandikisha Watoto wengi shule na kuboresha maslahi ya walimu.
Mkuu huyo wa UNICEF amesema hali ya sasa ni mbaya “Shule hazina rasilimali, walimu wanalipwa ujira mdogo, walimu wengine wasio na sifa wanaajiriwa, msongamano wa wanafunzi madarasani, mitaala ya kizamani na vyote hivi vinasababisha Watoto kushindwa kufikia uwezo wa juu wa ufaulu.”
 

Audio Duration
2'31"
Photo Credit
© UNICEF/Juan Haro