Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nitatumia ubalozi mwema kupaza sauti kwa maslahi ya watoto - Vanessa

Nitatumia ubalozi mwema kupaza sauti kwa maslahi ya watoto - Vanessa

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF leo limemteua na kumtangaza mwanaharakati wa mazingira kutoka nchini Uganda Vanessa Nakate kuwa balozi mwema mpya wa shirika hilo. 

Vanessa Nakate, Balozi mwema wa UNICEF, akiwa ziarani Turkana nchini Kenya alitembelea hospitali ya rufaa ya Lodwar na hapo anazungumza na mtoto Eunice Asukuku ambaye alifikishwa hospitali kwa tatizo la utapiamlo mkali, kuvimba mwili na ukosefu wa damu. Chanzo cha matatizo ni uhaba wa chakula utokanao na ukame uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Uteuzi wa Vanessa, mwenye umri wa miaka 25 unafuatia ziara yake kwenye Pembeme ya Afrika ambako alishuhudia jinsi gani mabadiliko ya tabianchi yalivyochangia athari mbaya kwa maisha ya watoto nchini Kenya kutokana na ukame unaoendelea.

Pia uteuzi huo ni kuthibitisha ushirikiano wake na shirika la UNICEF na kutambua utetezi wake bora wa kimataifa wa haki za kimazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Vanessa alisafiri wiki iliyopita na UNICEF hadi Kaunti ya Turkana Kaskazini Magharibi mwa Kenya ili kujionea athari za uhaba wa maji na chakula unaosababishwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika Pembe ya Afrika katika kipindi cha miaka 40. 

Katika safari yake ya kwanza na UNICEF, alikutana na jamii zilizo katika kitovu cha  athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kinamama na watoto wanaopata matibabu ya kuokoa maisha kutokana na utapiamlo mkali na familia zinazonufaika na mifumo ya usambazaji wa maji inayotumia nishati ya jua kwa msaada wa UNICEF.

Nitahakikisha sauti za watoto zinasikika

Baada ya kuteuliwa kwake Bi. Nakate amesema "Kama balozi mwema wa UNICEF, itakuwa jukumu langu la kwanza kuwasilisha sauti za watoto na watu waliotengwa katika mazungumzo ambayo awali hawakujumuishwa. Jukumu hili na UNICEF litanipa fursa zaidi za kukutana na watoto na vijana katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi na jukwaa lililopanuliwa la kutetea kwa niaba yao. Nchini Kenya, watu niliokutana nao waliniambia kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na ukame katika maisha yao, huku misimu minne ya mvua iliyofeli mfululizo ikiwanyima watoto haki zao za msingi.” 

Ameongeza kuwa  moja ya jamii alizokutana nazo imemweleza kuwa haijashuhudia mvua kwa zaidi ya miaka miwili. 

“Hii ni zaidi ya shida ya chakula na lishe, ni mwelekeo mwingine wa changamoto yetu ya mabadiliko ya tabianchi inayozidi kuwa mbaya.”

Ombi la UNICEF la kuboresha na kusaidia maisha ya mamilioni ya watu walioathirika na ukame na kuwajengea mnepo kwa muda mrefu kwenye Pembe ya Afrika na kuzuia athari za ukame kwa miaka ijayo zinagonga mwamba kwani hadi sasa ombi hilo limefadhiliwa kwa asilimia 3% pekee.

Akiwa Sopel, kaunti ya Turkana nchini Kenya, Vanessa Nakate alitembelea shule ya msingi na kuzungumza na wanafunzi kuhusu changamoto wanazozipata kutokana na janga la ukame kwenye eneo hilo la Afrika Mashariki.

Safari ya uanaharakati ya Vanessa Nakate

Vanessa alianza harakati zake Januari 2019 kwa maandamano na ndugu zake na binamu zake katika mitaa ya jiji la Kampala, nchini Uganda, maandamano yaliyochochewa na mwanaharakati mwingine nyota wa mabadiliko ya tabianchi na mazingira Greta Thunberg. Aliendelea kuandamana kila wiki, na kuwa sura inayojulikana katika harakati ya vijana kupiga mabadiliko ya tabianchi duniani kote. 

Mwaka 2020 alijulikana zaidi ulimwenguni wakati alipoondolewa kwenye picha ya habari aliyokuwemo pamoja na Thunberg na wanaharakati wengine weupe wa mabadiliko ya tabianchi. 

Kufuatia tukio hilo alochosema Vanessa ni kwamba chombo hicho cha habari "hakikufuta picha tu, bali kilifuta bara zima", kauli ambayo iligonga vichwa vya habari vya kimataifa.

Vanessa amesema safari yake haikuwa rahisi  “Kama mwanamke mwanaharakati mchanga wa Kiafrika, imenibidi kupigana ili kusikilizwa na vyombo vya habari na watoa maamuzi. Wakati nina bahati ya kuwa na jukwaa sasa, ninakusudia kuendelea kupigania wengine. Watoto walio katika kitovu cha athari za mabadiliko ya tabianchi, kama wale niliokutana nao Turkana, Kenya, ni watu ambao nitapigania katika jukumu langu jipya na UNICEF,” amesema Nakate.

Tangu wakati huo Vanessa ametumia jukwaa lake kutetea haki ya masuala ya mabadiliko ya tabianchi kujumuisha kila jamii, haswa wale kutoka sehemu zilizoathiriwa zaidi. 

Alianzisha Rise Up Movement, jukwaa la kupaza sauti za wanaharakati wa mabadiliko ya tabianchi wa Afrika, pamoja na mradi wa kufunga paneli za sola katika shule za vijijini za Uganda. 

Amehutubia viongozi wa dunia katika mikutano ya mabadiliko ya tabianchi ya COP25 na COP26 na alionekana na hadithi yake kuchapishwa kwenye jarida la TIME.

Audio Credit
FLORA
Sauti
4'29"
Photo Credit
© UNICEF/Translieu/Nyaberi