Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utumikishwaji kwenye kazi na kwenye ndoa vyaongezeka

Utumikishwaji kwenye kazi na kwenye ndoa vyaongezeka

Pakua

Watu milioni 50 walikuwa wakiishi katika utumwa wa kisasa mwaka jana 2021, kwa mujibu Ripoti ya hivi karibuni ya makadirio ya utumwa wa kisasa duniani ambayo imetolewa na shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa, ILO, Wakfu wa Walk Free na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM. Taarifa inayowasilishwa na Anold Kayanda ina maelezo zaidi. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo mjini Geniva nchini Uswisi, ILO, IOM na Wakfu wa Walk Free, makadirio ya hivi karibuni kupitia utafiti wao, yanaonesha kuwa kazi za kulazimishwa na ndoa za kulazimishwa zimeongezeka sana katika miaka mitano iliyopita. 

Watu milioni kumi zaidi walikuwa katika utumwa wa kisasa mwaka jana 2021 na hivyo kufikia watu milioni hamsini ikilinganishwa na makadirio ya kimataifa ya mwaka 2016. Wanawake na watoto wanabaki katika mazingira magumu kupita kiasi, umebaini utafiti.  

Kati ya watu hawa, milioni 28 walikuwa katika kazi ya kulazimishwa na milioni 22 wakiwa katika ndoa za kulazimishwa. 

Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy Ryder kwa amenukuliwa kwa maskitiko akisema, "inashangaza kwamba hali ya utumwa wa kisasa haibadiliki. Hakuna kinachoweza kuhalalisha kuendelea kwa ukiukwaji huu wa kimsingi wa haki za binadamu.”  

Ripoti imeonesha kuwa wafanyakazi wahamiaji wana uwezekano wa zaidi ya mara tatu kuwa katika kazi ya kulazimishwa kuliko wafanyakazi wazima wasio wahamiaji ndio maana Mkurugenzi Mkuu wa IOM, amesema, “ripoti hii inasisitiza udharura wa kuhakikisha kwamba uhamiaji wote ni salama, wenye utaratibu na wa kawaida." 

Taarifa imeeleza kuwa utumwa wa kisasa unatokea karibu kila nchi duniani, na unapita katika misingi ya kikabila, kitamaduni na kidini. Zaidi ya nusu (asilimia 52) ya kazi zote za kulazimishwa na robo ya ndoa zote za kulazimishwa zinaweza kupatikana katika nchi zenye kipato cha juu au cha kati. 

Audio Credit
Flora Nducha/ Anold Kayanda
Sauti
1'54"
Photo Credit
UN Women/Joe Saad