Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabwawa mchanga yametukomboa wanawake- Mkazi Tukrana, Kenya

Mabwawa mchanga yametukomboa wanawake- Mkazi Tukrana, Kenya

Pakua

Katika Kijiji cha Kanyangapus Kaunti ya Turkana nchini Kenya hali ya ukame ni mbaya sana kila kona na moja ya athari kubwa zilizoambatana nao ni ukosefu wa maji. 

Mabwawa ya mchanga yamekuwa suluhu bunifu inayozisaidia kaunti nyingi zilizo katika hali ya nusu jangwa nchini Kenya na shukrani kwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwa kufadhili wa mradi huo wa ujenzi wa mabwawa ya mchanga na pampu za maji, sasa adha ya maji katika kaunti ya Turkana imepungua na hususan kwa wanawake wanaolazimika kwenda umbali mrefu kusaka maji.  Happines Pallangyo wa Radio washirika Uhai FM kutoka Tabora anafafanua zaidi.
 
UNICEF imejenga mabwawa 10 ya mchanga katika kaunti ya Turkana na kuongeza fursa ya upatikanaji wa maji kwa katibu watu 6000, wa vijiji mbalimbali miongoni mwao ni Rebecca Anyuduk mama wa watoto watatu kutoka kijiji cha Kanyangapus.

Anna anasema walihaha sana kusaka maji kwa ajili ya watoto wao pamoja na mifugo yao akiongeza kuwa, « tulitembea hadi zaidi ya kilometa 10 ili kufika kulikokuwa na maji. Tulikuwa tunaishi mahali kulikokuwa na miti lakini tuliikata na baadhi kuichoma mkaa na kisha tunauuza ili kununua chakula.” 

Ukame unaoikabili kaunti ya Turkana haujawahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa, misimu minne ya mvua imefeli na kuna hatihati msimu wa tano nao mambo ni yale yale, sababu kubwa ikiwa ni mabadiliko ya tabianchi. Rebecca anasema amepoteza matumaini, mazao na hata mifugo yake sababu ya ukame huo.

Anafafanua “nilikuwa namiliki mifugo wengi lakini ukame ulipolikumba eneo hili baadhi ambao ni wengi walikufa nikabakiwa na mbuzi watato tu.” 

Athari za ukame Turkana

Jakson Mutia ni mtaalamu wa UNICEF wa masuala ya maji, usafi na kujisafi au WASH anasema ukame wa safari hii umeleta madhila makubwa.

Zaidi ya asilimia 30 ya wakaazi sawa na watu 360,000 hivi sasa hawana fursa ya maji salama, na wachache walio na fursa ya maji safi na salama wanalazimika kutembea wastani wa kilometa 9 kwenda na kurudi. 

Katika baadhi ya maeneo hakuna vyanzo vyovyote vya maji na hata maji ya ardhini hayapatikani, katika maeneo hayo inabidi tutumie njia bunifu tunachimba mabwawa ya mchanga.

Ameongeza kuwa bwawa la Kanyangapus lilijengwa mwezi Desemba mwaka jana na limekuwa mkombozi sio tu kwa watu wa Kijiji hicho  familia zao na mifugo yao bali pia vijiji vya jirani.

TAGS: Turkana, Kenya, UNICEF, Msaada wa Kibinadamu, ukame

Audio Credit
Flora Nducha/Happiness Pallangyo
Audio Duration
2'40"
Photo Credit
© UNICEF/Paul Kidero