Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asante ILO sasa naweza kuomba zabuni serikalini- Florence

Asante ILO sasa naweza kuomba zabuni serikalini- Florence

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO nchini Kenya, kwa kushirikiana na wadau wengine, hivi karibuni wamewaidhinisha na kuwakabidhi watu 62 vyeti vya kwanza kabisa vya RPL ambao ni mfumo wa kutambua, kutathmini na kuthibitisha maarifa na ujuzi au stadi za mtu bila kujali kwamba mtu huyo hakupita kwenye mfumo rasmi wa elimu. Taarifa ya Anold Kayanda inaeleza zaidi.  

“Mimi nilikuwa ninaogopa. Unajua watu ambao hawajasoma unaogopa mtihani,” akiwa amembeba mtoto wake mgongoni mbele ya umati uliofika kushiriki tukio hili, ni Florence Wambui mmoja wa waliohitimu kupitia mfumo huu wa RPL ambapo mtu aliye na ujuzi na uzoefu mkubwa kuhusu kazi fulani lakini hana vyeti, anatambuliwa na kupewa cheti. 

“Niliona ni muhimu kufanya RPL kwa sababu huko kwa Juakali hakuna vyeti, bali ni kufanya mambo kiujuakali tu (bila mfumo rasmi). Sasa nikaona ni muhimu kwenda kufanya mtihani nipate cheti. Unaona?!. Ndio hivyo hicho cheti kinaweza kunisaidia kupata tenda za serikali na pia kuinua kujiamini kwangu.” 

Naam na pia kuinua kujiamini kwake. Mwingine aliyetambuliwa ni Swaleh Rashid, mfanyakazi wa kampuni ya Base Titanium inayojihusisha na uchimbaji wa mchanga wa madini chuma nchini Kenya. Swaleh anahusika na masuala ya mitambo anasema, “nilikuja (hapa Base Titanium) nikiwa na ujuzi wangu ambapo nilikuwa nimechukua ufundi wa ngazi ya pili. Nilipoingia hapa, ikaja programu ya RPL ambayo niliipokea kwa mikono miwili kwa sababu niliona ina umuhimu kwangu. Nikachukua na nikakabidhiwa RPL kama fundi ngazi ya kwanza. Naninashukuru sana kwa maana naona hiyo ndio itanisaidia katika maisha yangu.” 

Dkt. Juma Kuhwama ni Mkurugenzi Mkuu wa KNQA ambayo ni Mamlaka nchini Kenya inayosimamia ubora wa mafunzo yote na sifa za kielimu zinazotolewa nchini Kenya anaeleza zaidi kuhusu utaratibu wa vyeti vya RPL yaani Recognition of Prior Learning akisema, “wengi wetu hatuna vyeti lakini tuna stadi au ujuzi. Tumejifunza kutoka kwa wazazi wetu, tumejifunza kutoka katika maeneo yetu ya kazi. Kwa hiyo wazo nyuma ya mfumo huu ni kuhakikisha kwamba tunakutathmini, tunakupa cheti ili kama unataka kuendelea na kazi yako, karatasi inaweza kukuruhusu kupata mikataba na serikali za kaunti, serikali kuu au kampuni ili uweze kuboresha maisha yako na pia unaweza kupata vyeti hivi na ukaendeleza elimu yako hadi ngazi ya uzamivu, PhD bila kupitia mfumo wa elimu ya sekondari. Hivyo ndivyo sheria inavyosema. Kwa hiyo ni mfumo muhimu sana. Lakini pia ambcho mfumo huu unatufanyia kimsingi ni kutambua ujuzi ambao mtu anao.” 

Audio Credit
Assumpta Massoi/ Anold Kayanda
Audio Duration
3'22"
Photo Credit
ILO Video