Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yataka usaidizi zaidi wa ulinzi kwa wakimbizi na wahamiaji

UNHCR yataka usaidizi zaidi wa ulinzi kwa wakimbizi na wahamiaji

Pakua

Pengo la huduma za ulinzi safari latumbukiza wakimbizi mikononi mwa wasafirishaji haramu

Kuelekea sikuya kimataifa dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu kesoh Julai 30, shirika la umoja wa Mataifa la wakimbizi duniani, UNHCR imesema ukosefu wa huduma za ulinzi kwa wakimbizi na wahamiaji wanaofanya safari hatarishi kutoka ukanda wa Sahel na Pembe ya Afrika kwenda Afrika Kaskazini na kisha Ulaya, kunawatumbukiza katika hatari ya mikono ya wasafirishaji haramu. Leah Mushi na taarifa zaidi.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo jijini Geneva ,Uswisi imenukuu ripoti yake inayomulika huduma za ulinzi kwa wasaka hifadhi, wakimbizi na wahamiaji wanapofanya safari ndefu, ripoti iliyotolewa leo mkesha wa siku ya kimataifa dhidi ya usafirishaji haramu binadamu.

UNHCR inasema baadhi yao wanakufa jangwani, wengine wanakumbwa na ukatili wa mara kwa mara wa kingono na kijinsia, kutekwa nyara hadi walipe kikombozi, mateso na aina mbali mbali za unyanyasaji wa kimwili na kisaikolojia.

Ripoti hiyo ya pili ya aina yake inaonesha mapengo yaliyoko kwenye huduma za ulinzi, kama vile malazi, kupata haki,kubaini manusura wa ukatili wa kijinsia na kingono, usafirishaji haramu na watoto wanaosafari bila wazazi au walezi.

Nchi 12 zimemulikwa kwenye ripoti hiyo nazo ni Burkina Faso, Cameroon, Chad, Cote d’Ivoire, Djibouti, Ethiopia, Mali, Mauritania, Morocco, Niger, Somalia, na Sudan.

Mjumbe maalum wa UNHCR kwa hali ya wakimbizi kwenye eneo la MEditeranea ya Kati na  Magharibi Vincent Cochetel amesema, “nasikitishwa sana na manyanyaso ambayo wakimbizi na wahamiaji wanakumbana nayo wanaposafiri kupitia ukanda wa Sahel na MAshariki na Pembe ya Afrika na wakati mwingine Ulaya. Vifo vingi vinatokea kupitia njia hizi.”

Bwana Cochetel amesisitiza umuhimu wa kutenga fedha zaidi kutekeleza huduma bora za ulinzi ili kuepusha usafirishaji haramu, kubaini na kusaidia manusura na kuhakikisha wanapata hifadhi sambamba na kufikisha watuhumiwa mbele ya sheria.

Ripoti inapatia wakimbizi na wahamiaji huduma zilizoko sasa kwenye njia mbalimbali wanazopita. Pia inatoa maelekezo kwa wahisani ni wapi wawekeze ambako kunahitajika zaidi.

Ili kusaidia manusura, ripoti inatoa wito kwa jamii ya kimataifa kuanzisha malazi ya kijamii na maeneo salama, halikadhalika huduma za kisheria na huduma tofauti tofauti kwa watoto na manusura wa kike.

TAGS: UNHCR, wahamiaji na wakimbizi, usafirishaji haramu wa binadamu
 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Audio Duration
2'23"
Photo Credit
Picha ya UNICEF/Alessio Romenzi