Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sanaa yatumika kuhamashisha amani DRC

Sanaa yatumika kuhamashisha amani DRC

Pakua
Huko Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, wasanii vijana wanatumia sanaa ya upakaji kuta rangi kama njia mojawapo ya kuhamasisha jamii kuachana na ghasia sambamba na kueneza kauli za chuki. Taarifa hii iliyoandaliwa na Esther Nsapu wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa huko DRC inasomwa studio na Assumpta Massoi. (Taarifa ya Assumpta Massoi) Nats.. Mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini, kuta za baadhi ya maeneo zimechorwa picha zenye ujumbe tofauti tofauti ! Mathalani Tusitupe mawe na tusichome matairi kwenye barabara ! Tunatakataa Ujeuri ! Tulinde na Tukinge mazingira. ! Ujumbe katika kuta hizi ni sehemu ya mradi wa Vijana Pamoja Jenga Nchi, au VIPAJI uliozinduliwa mwezi uliopita na Taasisi ya Sanaa ya Kivu, AKA, taasisi ambayo ni kituo cha tafiti za kitamaduni na ujasiriamali na makao yake ni Goma. Sanaa inaendelea ya uchorani ambapo AKA imekaribisha vijana wapendao sanaa hii kutoka mji wa Bukavu, jimboni Kivu Kusini, halikadhalika vijana kutoka mikoa jirani ya Rwanda kama vile Gisenyi. Mradi lengo lake ni kusongesha amani, kuondokana na ghasia, elimu ya uraia na kulinda mazingira. Thierry Vahwere Croki, mwenye umri wa miaka 37 ni miongoni mwa waanzilishi wa mradi huu na amekuweko kwenye sanaa hii kwa miaka 17 sasa anafurahi kufanya kazi na vijana kwa sababu vijana wanajipatia kipato na kwamba, (Sauti ya Thierry Croki) “Hawana muda wa kwenda kuombaomba au kubeba silaha kwa sababu wana kazi na wana kitu cha kufanya.” Na zaidi ya yote mradi ni muhimu kwa mji wa Goma wenye wakazi takribani milioni 2 kwa kuwa, (Sauti ya Thierry Croki) “Tunauvisha Goma vazi jipya! Michoro hii inapendezesha na siku hizo na teknolojia vijana wengi wana simu janja wakipita wanasoma ujumbe, wanapiga picha na kusambaza pia ujumbe kwa familia, ndugu na jamaa, shuleni na hivyo tunachora picha na kujisogeza karibu na jamii, vijana na wakati huo huo kuvunja fikra potofu.”
Audio Credit
Leah Mushi/ Assumpta Massoi
Photo Credit
UN News/ Esther Nsapu