Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mhamasishaji wa kijadi atumikisha kuchagiza chanjo Gambia

Mhamasishaji wa kijadi atumikisha kuchagiza chanjo Gambia

Pakua

Utoaji wa chanjo kwa watoto umekuwa unakumbwa na changamoto katika baadhi ya maeneo duniani kutokana na jamii kuwa na imani potofu na ndio maana huko nchini Gambia shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeamua kutumia washawishi kwenye jamii ili kuhamasisha wazazi kupeleka watoto wao kupata chanjo kama anavyosimulia Assumpta Massoi. 

Tuko nchini Gambia, taifa hili lililoko magharibi kabisa kwa Afrika, ni midundo ya ngoma kutoka kwa Lamine Keita, mwanamuziki wa kitamaduni, almaaruf, Takatiti. 

Kwa takribani miongo minne sasa ametumia ngoma yake moja anayoweka kwapani pamoja na kipaza sauti, akipita maeneo ya vijijini kuchagiza na kuhamasisha wazazi na walezi kupeleka watoto kupata chanjo. 

Bwana Takatiti mwenye umri wa miaka 60 anasema, “jukumu langu hii leo hapa kama mwanawawasiliano wa kijadi ni kujitokeza na timu ya watoa chanjo. Ninatumbuiza huku watoto wakipata chanjo. Tunapofika watu wanatoka haraka, hivyo tunatumbuiza kwa furaha na haraka tunatoa chanjo.” 

Na kweli kabisa, hapa wanawake na watoto wanaselebuka huku watoa chanjo wakiendelea na jukumu lao. 

UNICEF inasema kujengea imani wazazi na walezi kuhusu chanjo kama vile Polio, kunahitaji mtu kama Takatiti ambaye wanamfahamu na ambaye pia sauti yake wameizoea. 

Takatiti anasema, “kwa hiyo watu wanapenda chanjo sambamba na burudani.” 

Mwaka 2019, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO lilitangaza kuwa shaka na shuku dhidi ya chanjo ni miongoni mwa vitisho vya juu zaidi vya afya ya umma duniani.

Audio Credit
Leah Mushi/Assumpta Massoi
Audio Duration
1'37"
Photo Credit
© UNICEF/UN0624023/