Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunasherehekea watu wenye ualbino leo kwa sababu tumeona ujasiri wenu na bidii-Muluka Anne

Tunasherehekea watu wenye ualbino leo kwa sababu tumeona ujasiri wenu na bidii-Muluka Anne

Pakua

Ikiwa leo dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya kuelimisha jamii kuhusu watu wenye ualbino, Umoja wa Mataifa umetoa  rai kwa nchi zote duniani kuwajumuisha watu wenye ualbino katika mijadala na mipango inayoathiri haki zao za kibinadamu, ili kuhakikisha wanafurahia usawa na ulinzi unaotolewa kwao katika sheria na viwango vya kimataifa.

 Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu inasema ”Tuungane pamoja kufanya sauti zetu zisikike” ikihamasisha haja ya kufanya kazi pamoja na kujenga ushirikiano ili kukabiliana na changamoto za haki za binadamu zinazowakabili watu wenye ualbino.  

 Mtaalam Huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu ualbino Muluka-Anne Miti-Drummond amesema kupitia taarifa yake aliyotoa leo mjini Geneva Uswisi kuwa sehemu za kufanya maamuzi kuanzia ngazi za kimataifa, kitaifa , kijamii na hata katika sekta binafsi kumekosa uwakilishi wa watu wenye ualibino na hivyo wanashindwa kushiriki katika mijadala ya kufanya maamuzi na hali hiyo inaweza kusababisha ukiukwaji wa haki zao za kibinadamu.  

 Amesema,  “ni ubaguzi wa kimuundo na ukosefu wa usawa wa kihistoria. Hakuwezi kuwa na usawa bila kujumuishwa kwa sauti za walio hatarini zaidi. Ikiwa hatutajumuisha watu wenye ualbino katika majadiliano na maamuzi, tunaendeleza ubaguzi wa kimuundo na ukosefu wa usawa wa kihistoria.” 

 Hata hivyo ametoa pongezi akisema, 

"Tunasherehekea watu wenye ualbino leo kwa sababu tumeona ujasiri wenu na bidii. Tumeona ongezeko la idadi ya watetezi na wapiganaji wa haki za binadamu wenye ualbino, wengi wao ambao wameanzisha mashirika ya kirai wakati waliona haja ya uwepo wa watu wa kuleta mabadiliko. Wengi wenu mmefanya kazi bila kuchoka kukabiliana na mizizi ya unyanyapaa na mauji ya watu wenye ualbino ikiwemo kukabiliana na dhana potofu hatari kupitia kampeni za kuelimisha kwa kuchagiza ufikiaji wa huduma za afya na raslimali na kuhakikisha ujumuishaji katika shule na maeneo ya kazi ili kuongeza nafasi za watu wenye ualbino kupata mbinu za kujipatia kipato endelevu." 

 

Maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kuelimisha jamii kuhusu watu wenye ualbino mwaka huu pia yanasherehekea kazi zilizofanywa na vikundi vya wenye ualbino katika kupaza sauti zao nakuhamasisha kuendeleza mshikamano wakati wakiendelea kupambana kuhakikisha sauti zao zinasikika. 

Audio Credit
Leah Mushi/Grace Kaneiya
Audio Duration
2'24"
Photo Credit
UN News/Grece Kaneiya