Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

6 Mei 2022

6 Mei 2022

Pakua

Katika Jarida la Ijumaa Mei 6, 2022 na Leah Mushi

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO limezindua ripoti ya kwanza kabisa ya kimataifa kuhusu njia ya vitendo, yenye msingi wa ushahidi wa kulinda wagonjwa na wahudumu wa afya wasidhuriwe na maambukizi yanayoweza kuepukika. Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi. kupitia taarifa yake iliyotolewa hii leo jijini Geneva, Uswisi, WHO imesema janga la COVID-19 na milipuko mingine mikubwa ya maonjwa ya hivi karibuni imeonesha kiwango ambacho mipangilio ya huduma za afya inaweza kuchangia kuenea kwa maambukizi, kuwadhuru wagonjwa, wahudumu wa afya na wageni, ikiwa tahadhari ya kutosha haitaelekezwa katika kuzuia na kudhibiti maambukizi (IPC). Pia ripoti hiyo mpya inaonesha kuwa pale ambapo usafi mzuri wa mikono na taratibu nyingine za gharama nafuu zinafuatwa, asilimia 70 ya maambukizi hayo yanaweza kuzuilika. 

===================================================================================  

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO, katika ripoti yake ya hali ya bei ya vyakula duniani iliyotolewa mjini Roma, Italia leo, limesema bei za bidhaa za chakula duniani zilipungua mwezi Aprili baada ya kupanda kwa kiwango kikubwa mwezi wa Machi, ushukaji huu ukiongozwa na kushuka kidogo kwa bei ya mafuta ya mboga na nafaka, huku bei ya mchele, nyama, maziwa na sukari ikiongezeka kidogo na matarajio ya biashara ya kimataifa yakififia. Mchumi Mkuu wa FAO Máximo Torero Cullen amesema, "kupungua kidogo kwa bei ni afueni inayokaribishwa, hasa kwa nchi za kipato cha chini zenye upungufu wa chakula, lakini bado bei za vyakula zinasalia kuwa karibu na viwango vya juu vya hivi karibuni, jambo linaloakisi mkwamo wa soko na kuleta changamoto kwa uhakika wa chakula duniani kwa walio hatarini zaidi.” 

===================================================================================== 

Na Shirika la posta duniani, UPU, limezindua njia ya ziada kwa ajili ya kutoa usaidizi kwa Posta ya Ukraine, (Ukrposhta) kupitia Mfuko wake wa Ubora wa Huduma. Ukrposhta imeendelea kuwasilisha misaada ya kibinadamu, malipo ya pensheni na huduma nyingine za posta katika muda wote wa mzozo huo, licha ya kupoteza maisha na kujeruhiwa kwa wafanyakazi wa posta, pamoja na uharibifu wa mali na miundombinu ya Posta. Taarifa iliyotolewa mjini Bern, Switzerland imemnukuu Mkurugenzi Mkuu wa UPU, Masahiko Metoki akisema, "mshikamano ni kanuni ya msingi ya UPU. Wenzetu katika Ukrposhta wameomba msaada wetu na lazima tujibu ili kuhakikisha watu na jamii zinaendelea kupokea misaada ya kibinadamu na huduma nyingine muhimu zinazotolewa na Posta. Kwa hivyo natoa wito kwa familia yetu ya posta kusaidia wenzetu nchini Ukraine kwa njia yoyote iwezekanayo, ikijumuisha kupitia njia hii mpya.” 

======= 

Katika mada kwa kina ni kijana aliyegeukia ubunifu baada ya kukosa kazi licha ya kuhitimu kutoka chuo kikuu nchini Tanzania.

Katika neno la wiki inachambuliwa methali “KOSA MOJA HALIMWACHI MKE” 

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
12'38"