Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Toxorhynchites

Toxorhynchites

Pakua

Dokta Jovin Kitau kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO nchini Tanzania, ambaye ni mtaalamu wa kudhibiti na kufuatilia ugonjwa Malaria anasema Toxorhynchites wamebainika katika tafiti kuwa wanakula mbu wengine.

“Tafiti zinaonesha kuwa mbu hao wanapokuwa bado ni viluilui wana uwezo wa kula viluilui wa mbu wengine akiwemo aina ya Anopheles ambayo ndio inaambukiza Malaria. Kwa hiyo hizi ni tafiti ambazo zimeweza kuthibitisha kuwa aina hii ya mbu inaweza kuongezwa kama sehemu ya mkakati ya kuzuia mbu waenezao Malaria,” amesema Dokta Kitau akihojiwa na Filbert Alexander wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa, UNIC jijini Dar es salaam, nchini Tanzania.

Hata hivyo mtaalamu huyo amesema “hakujawa na majaribio ya kutosha ya kuwezesha kutambua kama kweli mbinu hii ya kutumia mbu kula mbu wengine inaweza ikaleta manufaa kwenye kupunguza maambukizi  ya vimelea vya Malaria kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine kupitia mbu.”

Amesema ni kwa sababu ya kukosekana kwa taarifa na takwimu zinazoweza kuhusianisha moja kwa moja, “kwa maana ya kwamba kupunguza mbu waenezao Malaria kwa kutumia mbu wengine, hii inaifanya kuwa ni mbinu inayoweza kutumika lakini haijafanikiwa kutangazwa sana kama mbinu za kutumia vyandarua na kupulizia dawa za ukoko na kadhalika.”

Audio Credit
Dokta Jovin Kiatu
Audio Duration
1'28"
Photo Credit
Sven Torfinn/WHO 2016