COVID-19 imepukutisha kipato cha familia zenye watoto
Tangu kuanza kwa janga la ugonjwa wa Corona au coronavirus">COVID-19 mwaka 2020, kaya mbili kati ya tatu duniani kote zenye watoto zimepoteza vipato, imesema ripoti mpya iliyochapishwa leo na Benki ya Dunia na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF. Taarifa kamili inasomwa na Assumpta Massoi.
Ni Sibongile Matume huyo, mkazi wa bustani ya Freedom jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini, akijitambulisha katika video ya UNICEF. COVID-19 imemuondosha kazini na sasa hana ujira, amefika katika kituo kupokea fedha za kujikimu yeye na watoto wake.”
Sibongile na familia yake ni miongoni mwa familia 2 kati ya 3 ambazo ripoti iliyozinduliwa leo inasema kuwa zimepoteza njia ya kujipatia kipato.
Ikipatiwa jina madhara ya COVID-19 katika ustawi wa kaya zenye watoto, ripoti inawasilisha takwimu za utafiti kutoka nchi 35 ikisema kaya zenye watoto watatu au zaidi zilikuwa katika nafasi ya kupoteza kabisa kipato au zina uwezo wa robo tatu zaidi kupata pungufu la kipato, kiwango ambacho ni cha juu ikilinganishwa na kaya zenye mtoto mmoja au wawili.
Ripoti imesema pia kupotea kwa kipato kumesababisha watu wazima katika kaya 1 katika kila kaya 4 kushinda siku nzima au zaidi bila mlo, huku kaya nyingine zikivuka milo mingine kutokana na ukata.
Takribani robo ya watu wazima katika kaya zenye watoto au bila watoto waliacha kufanya kazi wakati COVID-19 ilipoanza.
Mkurugenzi wa miradi wa UNICEF Sanjay Wijesekera anasema kwa hali hii ina maana “maendeleo kidogo yaliyofikiwa duniani katika kupunguza umaskini hivi karibuni yako hatarini kufutika. Familia zimepata hasara kwa kiwango kikubwa. Familia haziwezi kumudu kununua chakula au huduma muhimu za afya, haziwezi pia kumudu makazi. Ni taswira ya kusikitisha na kaya maskini zinasukumwa zaidi katika lindi ya ufukara.”
Carolina Sánchez-Páramo, afisa kutoka Benki ya Dunia anasema kuvurugwa kwa elimu na huduma za afya kwa watoto kunaweza kukwamisha maendeleo ya rasilimali watu katika viwango vya elimu, afya na ustawi wa watu ambavyo ni muhimu kwa wao kuwa washiriki bora kwenye maendeleo ya mataifa yao.
Hali hiyo amesema inaweza kuongeza ukosefu wa usawa katika vizazi vijavyo na kwamba watoto hawatakuwa na uwezo wa kuwa bora zaidi kuliko wazazi au bibi na babu zao.
UNICEF na Benki ya Dunia zinasihi upanuzi wa haraka wa mifumo ya hifadhi ya jamii kwa watoto na familia zao. Msaada huo ujumuishe upatiaji wa familia fedha taslimu na kuweka mpango wa huduma za maslahi ya watoto kuwa kwa kila mtu ili kusaidia familia kujinasua wakati wa majanga.