Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hitaji la dharura kuboresha mifumo ya udhibiti wa taka laonekana baada ya taka zilizotokana na kudhibiti COVID-19 kuwa tishio

Hitaji la dharura kuboresha mifumo ya udhibiti wa taka laonekana baada ya taka zilizotokana na kudhibiti COVID-19 kuwa tishio

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO limetoa ripoti mpya inayoonesha kuwa mifumo ya usimamizi wa taka za afya duniani kote hivi sasa imezidiwa uwezo kutokana na maelfu ya tani za taka zinazotokana na vifaa vilivyotengenezwa kwa ajili ya kukabiliana na janga la COVID-19 na hivyo kutishia afya ya binadamu na mazingira na wakati huo huo kufichua hitaji kubwa la kuboresha udhibiti wa taka zinazozalishwa kutokana na huduma ya tiba.  

Dkt. Margaret Montgomery, Afisa wa Kiufundi wa WHO Kitengo cha Maji, Kujisafi, Usafi na Afya akizungumzia ripoti hiyo akiwa katika makao makuu ya shirika hilo mjini Geneva, Uswisi amesema,"kwa hivyo, matokeo makuu ya utafiti ni kwamba kuna taka za ziada zinazozalishwa. Ni mara tatu hadi nne ya kiwango cha taka ambacho kimezalishwa wakati wa janga hili la Covid-19. Na katika vituo ambavyo havitenganishi taka, idadi hiyo inaongezeka hadi mara 10. Wakati huo huo, wakati  tunafahamu kuwa vituo vya afya vinazidiwa nguvu kushughulikia suala hili la taka.” 

Kuhusu ushauri wa WHO wa jinsi ya kulishughulikia tatizo hili la taka, Dkt. Montgomery anasema,"kwa hivyo kitu cha kwanza ni kutotumia vifaa tiba ambayo haihitajiki. Kwa mfano Glovu hazihitajiki wakati wa chanjo na hazihitajiki katika matibabu mengi achilia mbali kwa umma. Kwa hivyo ikiwa tunaweza kupunguza glovu katika nchi, kama Uingereza, ambayo tayari ilikuwa na kampeni ya kutotumia glovu hata kabla ya COVID- 19, itakuwa vizuri sana.” 

Aidha afisa huyo wa WHO ametaja njia nyingine ya kupambana na taka zizazotokana na vifaa tiba kuwa ni pamoja na kuanza kufikiria matumizi ya karatasi katika vifungashio, urejereshaji wa baadhi ya taka na namna ambavyo vitu kama barakoa na vifaa vingine vinaweza kutumiwa tena katika uzalishaji wa bidhaa nyingine mathalani vifaa vya ujenzi.   

Na kuhusu ni ujumbe gani anao, Dkt. Margaret Montgomery anasema,"ujumbe ni kwamba hatuwezi tena kupuuza suala la taka. Habari njema ni kwamba tunaweza kukinga na kuzuia dhidi ya COVID-19 na tunaweza kulinda mazingira. Kwa hivyo mambo kama kupunguza matumizi ya vifaa vya kujikinga wakati wa tiba visiyo vya lazima, mambo kama kutumia tena vifaa ambavyo ni salama, hasaa kwa umma mahali zilipo, kama barakoa. Na suala la tatu ni kuwekeza zaidi katika mifumo ya taka na wafanyakazi wa kushughulikia taka ili kuhakikisha kuwa suala hili linashughulikiwa kwa usalama na uendelevu." 

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
2'44"