Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sophie afurahia mradi wa UNHCR ulivyomnusuru kiuchumi ukimbizini

Sophie afurahia mradi wa UNHCR ulivyomnusuru kiuchumi ukimbizini

Pakua

Nchini Cote d’Ivoire  shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limeleta tabasamu na nuru kwa wakimbizi ambao biashara zao zilivurugika kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 ambalo limetikisa dunia kuanzia mwaka jana wa 2020. Kwa sasa wakimbizi hao wakiwemo wa kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC wana imani ya kujiinua tena kiuchumi kama anavyosimulia Happiness Pallangyo wa Radio washirika Radio Uhai FM ya Tabora Tanzania katika taarifa hii iliyoandaliwa na UNHCR.
“Mimi ni mtaalamu wa kusafisha Samaki,” ndivyo asemavyo Sophie Lilombi Mwika, mkimbizi kutoka DRC ambaye sasa anaishi kwenye mji mkuu wa kibiashara wa Cote d’Ivore, Abidjan. 
Katika video ya UNHCR, Sophie akiwa nyumbani kwake akiandaa Samaki anaokausha kwa chumvi anasema “naipenda kazi hii kwa sababu kupitia biashara ya samaki nimeondokana na umaskini.”
Sophie alikimbia DRC kutokana na ghasia na hapa Cote D’Ivoire akaanza biashara ya samaki wakavu. Akiwa anakagua vitabu vyake vya mahesabu ya biashara anasema, “COVID-19 imeniumiza sana. Ni kama vile imenichapa kiboko kama tusemavyo nchini mwetu DRC. Biashara ilipungua.”
Sophie alikuwa anauza Samaki wakavu siyo tu nchini Cote D’Ivoire bali pia nchi jiran ikiwemo ya Mali. Fedha alizopata aliweza pia kutuma nyumbani DRC kwa familia yake na hata alikuwa amepanga kupanua eneo la kuhifadhi samaki.
Hata hivyo ujio wa COVID-19 ukalazimu nchi kufunga mipaka ambapo mauzo yalipungua kwa theluthi tatu na hivyo akasitisha mpango wa kupanua ujenzi wa eneo la kuhifadhi samaki.
Mungu si Athumani, wahenga wamenena! UNHCR ikaingilia kati na kumpatia Sophie na wakimbizi wengine 80 mafunzo ya kuinua upya biashara zao sambamba na fedha taslimu za mtaji.
Leonidas Nkurunzinza ni Naibu Mwakilishi wa UNHCR nchini Côte d’Ivoire:
“Idadi kubwa ya watu tunaowasaidia wameathirika zaidi kuliko wengine. Hii ni kwasababu wako kwenye sekta isiyo rasmi, wakifanya biashara ndogo za kujikimu.”
Na sasa kwa Sophie mambo ni mazuri akisema “mimi ni mwanamke thabiti hii leo kwa sababu ya biashara yangu ya Samaki wakavu. Ninajivunia na ninajivunia kile nilichoanzisha. Tuko huru kufurahia maisha.“
Ama hakika furaha hadi kuimba na kucheza!
 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Happiness Pallangyo
Sauti
2'39"
Photo Credit
© FAO Cameroon