Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yajivunia ushirikishaji vijana kwenye kilimo

FAO yajivunia ushirikishaji vijana kwenye kilimo

Pakua

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO Qu Dongyu ametoa ujumbe wake kwa mwaka mpya wa 2022 huku akitaja mafanikio ambayo shirika hilo limefanikisha mwaka huu wa 2021 licha ya changamoto ya janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19.
Katika salamu hizo kwa njia ya video Bwana Qu amesema mafanikio hayo ni pamoja na mikutano waliyoendesha ili kufanya kazi usiku na mchana kuleta mabadiliko yanayoweza kuondoa njaa duniani.
“Jukwaa la dunia la chakula lilifanyika wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba likichochewa na kamati ya vijana ya FAO, na lilileta pamoja maelfu ya vijana wenye vipaji ili kubonga bongo na kubuni jinsi ya kubadili mifumo ya chakula duniani kwa mustakabali bora. Dunia ijayo ni ya vijana na inategemea vijana wa leo. Siku ya chakula dunia mwaka 2021 ilibeba maudhui vitendo vyetu mustakabali wetu, mifumo ya chakula inaanza na mimi. Sote tunapaswa kuwa mashujaa wa chakula.”
Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO akagusia pia mpango wa vijiji 1000 vya kidijitali akisema, “Mpango wa FAO wa vijiji 1000 vya kidijitali unawezesha wakulima kutumia teknolojia mpya kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo na kuondoa pengo la kidijitali. Sayansi na ubunifu ni msingi wa uhakika wa chakula.”
Amesema kwa mwaka 2022 wataendelea kutoa huduma bora zaidi na za kipekee ili kufanikisha mambo makuu manne bora ambayo ni Uzalishaji Bora, Lishe Bora, Mazingira Bora na Maisha bora kwa kila mtu bila kumwacha nyuma mtu  yeyote.
Kwa mujibu wa FAO janga la COVID-19 na kudorora kwa uchumi kumetumbukiza watu wengi kwenye machungu na duniani kote zaidi ya watu milioni 800 wana njaa na kati yao milioni 45 wako hatarini kufa njaa.
 

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
1'47"
Photo Credit
FAO Tanzania