Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utani baina ya makabila ni moja ya mbinu za kuchagiza amani na maelewano

Utani baina ya makabila ni moja ya mbinu za kuchagiza amani na maelewano

Pakua

Tofauti zinapaswa kuimarisha jamii badala ya kuisambaratisha, huo ndio  ujumbe uliotamalaki wakati wa kampeni iliyoendeshwa nchini Mali na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini humo MINUSMA kwa kushirikiana na chama cha wadau wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MANU. Kampeni ilileta pamoja wazee kwa vijana, wanawake kwa wanaume pamoja na Watoto wenye vipaji vya Sanaa na utamaduni. Nini kilifanyika, tujiunge na Jason Nyakundi katika taarifa hii.
Utamaduni na sanaa kutoka makundi mbalimbali vilishamiri kwenye tamasha hili la utamduni kwa ajili ya amani kwenye viunga vya mji mkuu wa Mali, Bamako. Ilikuwa ni ngoma, nyingine zikitumia vikaragosi.
Chifu wa Kijiji cha Koulouninke Adama Coulibally anasema “ukienda njia mbaya unakuwa hatarini kufika eneo hatarishi. Matamanio yetu ni kwamba katu tusiende njia mbaya. Hicho ndio tumejifunza kutoka kwa wazee wetu. Tunapaswa kupeleka ujumbe huu kwa watoto wetu na marafiki zetu. “
Abdoula Toure, afisa kutoka kitengo cha mawasiliano MINUSMA anasema, “Mali ni nchi kubwa na yenye makabila na tamaduni nyingi tofauti tofauti. Sisi Umoja wa Mataifa tunatambua hilo na ndio  maana tunapatia umuhimu matumizi chanya ya tofauti hizo ili kuleta utangamano.” 
Kwa Madani Diabate ambaye ni mhifadhi wa turathi za kiasili anasema “tofauti za kitamaduni na kikabila nchini Mali zinapaswa kutumika kujenga amani. Kupitia huo utofauti ndio tunaleta utani baina ya makabila na kisha ujirani mwema. Hicho ndio kinaweza kuimarisha amani na kujenga utangamano baina yetu.”
Wanawake ambao wamekuwa wakitaabika zaidi kutokana na machafuko nchini Mali nao wakapaza sauti kupitia Fatoumata Traore, mshauri wa kijamii mjini Bamako.“Ujumbe ambao naupaza kila wakati ni kwamba wanawake lazima wajumuishwe. Inapaswa wanawake nchini Mali watambue kuwa Mali ni moja na haigawanyiki. Kazi hiyo tunapasa kuifanya na tutaikamilisha.”
Na ili kuishi pamoja, wananchi wa Mali wafanye nini? Baba Salah Cisse, mwanamuziki aliyeshiriki kampeni hiyo akatoa ujumbe kupitia wimbo akisema, “Ili kuishi pamoja tunapaswa kukubaliana na kusameheana! Kama huna jinsi, muombe msamaha jirani yako! Kama hatutasameheana, amani haiwezi kupatikana. Na bila amani hakuna maendeleo.”
 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Jason Nyakundi
Audio Duration
2'39"
Photo Credit
MINUSMA/Harandane Dicko