Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto mapacha Yemen watenganishwa kwa msaada wa wahisani na UNICEF

Watoto mapacha Yemen watenganishwa kwa msaada wa wahisani na UNICEF

Pakua

Mapacha wawili waliozaliwa huko Sana’a nchini Yemen wakiwa wameungana kuanzia kifuani hadi tumboni hatimaye wametenganishwa huko Jordan na wamerejea nyumbani. Taarifa ya Happiness Pallangyo wa radio washirika Uhai Radio FM kutoka Tabora inafafanua zaidi.

Ahmed na Mohammed walizaliwa mwezi Desemba mwaka jana wa 2020 wakiwa wameunganika kifua na tumbo, hali ambayo ililazimu madaktari mjini Sana’a kuomba usaidizi kutoka UNICEF ili wasafirishwe kwa ndege hadi Jordan kwa ajili ya upasuaji wa kutenganishwa. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF lilichangisha fedha za kufanikisha upasuaji huo uliofanyika kwenye mji mkuu wa Jordan, Amman. 

Upasuaji ulinfanyika mwezi Julai katika hospitali maalum mjini Amman, na baada ya miezi kadhaa ya kupata matibabu na kupona hatimaye wamerejea nyumbani Yemen. 

Upasuaji huo umefanikishwa kutokana na ukarimu wa wahisani mbalimbali binafsi. 

Katika uwanja wa ndege wa Sana’a wazazi wa watoto hao hawakuficha tabasamu yao baada ya kuwabeba watoto wao mikononi mwao. 

Mwakilishi wa UNICEF nchini Yemen Philippe Duamelle amesema wahisani binafsi na timu ya madaktari katika hospitali mjini Amman samamba na mamlaka za Jordan vimefanikisha upasuaji huo. 

Hata hivyo amesisitiza kuwa ingawa simulizi hiyo imekuwa ya matumaini kwa familia hiyo moja ya mapacha hao, bado mamilioni ya watoto nchini Yemen wanaendelea kutaabika kimya kimya. 

Ametaja mahitaji mengine kuwa ni elimu, ulinzi na huduma kama vile maji. 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Happiness Pallangyo
Audio Duration
1'48"
Photo Credit
© UNICEF/UN0565880/YPN