UNICEF yasaidia watoto wenye utapiamlo Garissa nchini Kenya

UNICEF yasaidia watoto wenye utapiamlo Garissa nchini Kenya

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linaendesha program maalum ya lishe kwenye kaunti ya Garissa nchini Kenya kwa lengo la kunusuru maisha ya mamia ya watoto wanaosumbuliwa na utapiamlo. Jason Nyakundi na taarifa zaidi 

Nattsss…. 
Katika kaunti ya Garissa nchini Kenya ukame umetamalaki na kuathiri sio tu mifugo bali wananchi wa eneo hili wakiwemo mamia ya watoto  ambao sasa wana utapiamlo kama anavyosema Shahmat Yusuf mratibu wa lishe katika kaunti hii 
“Katika kaunti ya Garissa ukame umetuathiri sana kiasi kwamba tuko katika mgogoro, na vyanzo vyote vya maji vimekauka hivyo hii ndio hali halisi. Watu wengi wamehama kutoka kwenye vijiji vyao na kukimbilia mjini na watoto wengi wameathirika. Katika kila watoto 100, kumi na saba kati yao wana utapiamlo na endapo mvua haitonyesha basi hali itakuwa mbaya zaidi” 

Mmoja wa wazazi Kah Hassan anasema ilimlazimu kukimbia kwenda kuishi na ndugu mjini maana hakuwa na maji wala chakula cha kulisha watoto wake ambao ni wadogo na hakuweza kulipa kodi ya pango. 

Lakini sasa kupitia kampeni na mradi wa lishe wa UNICEF kwa kushirikiana na wizara ya afya ya Kenya na maafisa lishe wa kaunti wanapita nyumba kwa nyumba kupima watoto na kutoa mapendekezo ya kuwasaidia wale wenye utapiamlo kama anavyofanya afisa wa afya ya jamii wa kujitolea Mohammed Omar  ambaye anasema “Nilipomtembelea Kah nyumbani niliwapima watoto wake na nikamshauri awapeleke hospitali kwa sababu walikuwa na utapiamlo.” 

Mbali ya huduma UNICEF inasaidia pia kutoa chakula chenye lishe kwa watoto na mafunzo kwa wahudumu wa afya ya jamii  ili kuweza kukabiliana na changamoto za utapiamlo. 

Mafunzo wanayotoa yamekuwa mkombozi kwani yanawasaidia sana wahudumu wa afya kubaini watoto walio na utapiamlo na kuwapa matibabu yanayostahili lakini pia kwa wazazi imekuwa faraja ya kuwaondolea hofu ya kupoteza watoto wao kwa ugonjwa ambao unatibika. 

Audio Credit
Flora Nducha/ Jason Nyakundi
Sauti
2'4"
Photo Credit
Eric Omondi, muuguzi wa Kituo cha Usimamizi na Taarifa za Kisukari anakagua eneo lenye uvimbe kwenye mkono wa Maingi.