Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano wa kijeshi kati ya DRC na Tanzania wapongezwa

Ushirikiano wa kijeshi kati ya DRC na Tanzania wapongezwa

Pakua

Ushirikiano kati ya vyombo vya usalama ikiwemo polisi na FRDC ambalo ni Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na vikosi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu chini ya Mwavuli wa MONUSCO, umeendelea kuzaa matunda kwa kuwahakikishia usalama wananchi wa maeneo ya mashariki mwa DRC.

Miongoni mwa vikosi hivyo ni vile vya askari kutoka Tanzania yaani kikosi cha 8 cha kujibu mashambulizi kutoka TANZBATT-08 na TANZQRF -01 ambacho ni kikosi cha kuchukua hatua za haraka yaani Quick Reaction Force. 
Meya wa mji wa Beni, Kanali Narisce Muteba Katale kwa niaba ya wananchi wenzake anasema angependa kuona askari hao wakibaki hapo hadi amani itakaporejea,

"Tunaishi pamoja na kazi inaendelea vizuri tunafanya kazi pamoja. Kusema ukweli ningependelea waendelee kukaa hapa ili jinsi amani ilivyo Tanzania ndivyo na amani ije hapa (DR)Congo, itakuwa kitu kizuri zaidi. Serikali, MONUSCO na watu wote, ni salama zaidi"

Kauli ya Meya wa mji wa Beni inaungwa mkono na mkazi wa mji huu wa Beni ambaye amejitambulisha kwa jina moja la Josephine. Josephine anasema ushirikiano kati ya DRC na Tanzania uendelee kwa askari hao kuendelea kuwepo,

"Ninajisikia vizuri hakuna shida kabisa. Ninawatakia kazi njema watusaidie kupigana vita ya hapa kwetu Congo ili tuweze kupata amani."

Luteni Kanali Enock Masagasi ni Mkuu wa Kikosi cha Tanzania cha kuchukua hatua za haraka, TANZQRF-01 anawahakikishia uasalama wananchi wa DRC kwa kuwa ushirikiano wanaoupata ni mkubwa,

"Ushirikiano kati yetu na jeshi la Congo ambao ni FRDC pamoja na vyombo vyote vya ulinzi na usalama vya Congo ni mzuri. Kwanza napenda kusema kuwa tunazo tamaduni ambazo zinafanana,tunaongea lugha moja kwa hivyo inakuwa rahisi na vyepesi sana kwetu sisi kuweza kuwa nao katika majukumu mbalimbali kwa sababu tunaweza kuelewana katika maongezi yetu pia kuelewana katika mazoezi na peresheni mbalimbali ambazo tumekuwa tukishiriki kwa pamoja kuweza kutokomeza hili tatizo la waasi."

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'11"
Photo Credit
TANZBATT 7/Ibrahim Mayambua