Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshindi wa tuzo ya mazingira wa UNEP 2021 kutoka Uganda azungumzia kazi anazofanya

Mshindi wa tuzo ya mazingira wa UNEP 2021 kutoka Uganda azungumzia kazi anazofanya

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa mazingira duniani, UNEP wiki hii Jumanne ya tarehe 07 limewatangaza washindi wanne wa tuzo yake ya juu kabisa ya mazingira ijulikanayo kama “champions of the Earth Award” kwa mwaka 2021. Mabingwa hao walichaguliwa kutokana na mchango katika mazingira na uongozi wao katika kuendeleza hatua za ujasiri na madhubuti kwa niaba ya watu wengine wa sayari dunia. Dk Gladys Kalema-Zikusoka wa Uganda ni mmoja wa tuzo hiyo ya UNEP katika kipengele cha Sayansi na Ubunifu.

Taarifa zaidi anayo mwandishi wetu wa Uganda, John Kibego.

“I'm Dr. Gladys Kalema-Zikusoka” 
Ni Dkt Gladys Kalema-Zikusoka, mwanzilishi na Mkurugenzi wa shirika lisilo la kibiashara la ‘Conservation Through Public Health’.  Yeye ni daktari wa wanyamapori na mhifadhi na anasema amekuwa akiwahudumia wanyama sokwe kwa miaka 25. 

Dkt. Kalema-Zikusoka ni daktari wa wanyamapori wa kwanza kabisa wa Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda, mamlaka inayotambulika duniani kuhusu Wanyama wa asili hiyo ya nyani na pia magonjwa yatokanayo na Wanyama. Kupitia shirika lake hilo la Uhifadhi Kupitia Afya ya Umma, anaongoza utekelezaji wa programu tatu za kimkakati jumuishi kwa kutumia mbinu ya ‘Afya Moja’. 

"Kwa kuniajiri kama daktari wa kwanza wa Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda. Nimekuwa daktari wa wanyamapori wa muda wote nchini Uganda, na hilo lilianza kuwafanya watu watambue kwamba ustawi wa wanyama ni muhimu katika uhifadhi.” 

Mbinu ya ‘Afya Moja’ ambayo anaitumia Dkt Kalema-Zikusoka na shirika lake, inalenga kwa pamoja kuleta uhusiano mzuri kati ya Wanyama, wanadamu na mazingira bila kundi moja kuliathiri jingine. "Njia ya afya moja inashughulikia afya ya wanadamu, wanyama na mazingira kwa pamoja." Anasema Dkt Kalema-Zikusoka. 
Wataalam wa afya wanapita mstuni na kufanya utafiti na pia wanazungumza na wanajamii wa eneo hilo. Dkt Kalema-Zikusoka anafafanua zaidi kuhusu hilo. 

"Kwa hivyo, tunaona kwamba tunahitaji kuboresha ustawi wa jamii. Na njia moja tunayofanya ni kuboresha afya zao, ambayo pia hulinda sokwe.” 

Uhusiano mzuri kati ya watu, mazingira na wanyama, una mchango mkubwa katika kuondoa uwezekano wa magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa wanadamu au kinyume chake. Jamii inashirikishwa katika kuwatunza Wanyama ili waishi kwa afya.  Dkt Gladys Kalema-Zikusoka tena, 

"Tunajenga jamii ya wanywaji kahawa katika mgahawa wetu wa kuhifadhi sokwe. Tunanunua kahawa kutoka kwa wakulima wanaopakana na hifadhi tu. Kwa hivyo, kwenye mgahawa wa kuhifadhi sokwe watu wanajua kwamba wanapokuja na kununua kahawa pale au kunywa kahawa hapo, wanajua kwamba wanasaidia kuokoa sokwe.” 
Dkt Kalema-Zikusoka anasema wana timu ya walinzi wa sokwe. Haw ani wasuluhishi wa mgogoro kati ya wanadamu na soke.

"Pindi jamii hizi za wenyeji zinapowaona sokwe kwenye bustani zao, wanaweza kuwaita walinzi wa sokwe wanaoishi katika vijiji ambako masokwe hutoka na watawachunga na kuwarejesha mstuni kwa usalama bila kumuumiza yeyote." 

Tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 2005, tuzo ya kila mwaka ya Mabingwa wa Dunia, tuzo ya juu kabisa ya mazingira ya Umoja wa Mataifa, imetunukiwa baadhi ya viongozi mahiri wa mazingira duniani. Hadi sasa, imetunukiwa kwa washindi 101, wakiwemo viongozi 25 wa dunia, watu 62 na mashirika 14. Mwaka huu, UNEP ilipokea idadi ya idadi ya juu ya uteuzi kutoka kote ulimwenguni. 
 

Audio Credit
John Kibego
Sauti
3'39"
Photo Credit
UNEP