Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yasema baada ya juhudi za miaka 75 hali inarudi kuwa mbaya kwa watoto sababu ya COVID-19

UNICEF yasema baada ya juhudi za miaka 75 hali inarudi kuwa mbaya kwa watoto sababu ya COVID-19

Pakua

Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF imesema janga la COVID-19 limeleta hali mbaya zaidi kwa watoto kuwahi kushuhudiwa katika historia yake ya miaka 75 nakuzitaka nchi kuongeza juhudi kuwanusuru watoto.

Leah Mushi na taarifa zaidi. 
Ripoti hiyo iliyopewa jina la Kuzuia muongo uliopotea: Hatua ya haraka ya kubadili athari mbaya ya COVID-19 kwa watoto na vijana imetanabaisha kuwa hali ya watoto katika maeneo mengi duniani ilikuwa mbaya, lakini miaka miwili ya janga la Corona au COVID-19 limeididimiza zaidi na kuwaweka watoto hatarini zaidi kwakuongeza changamoto za umasikini, lishe, afya ya akili, ukosefu wa usawa na kuongezeka kwa umasikini. 

Akisoma ripoti hiyo jijini New York, Marekani Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema licha ya historia yao nzuri ya kuunda mazingira bora na salama kwa watoto ulimwenguni na matokeo kuwa mazuri kwa mamilioni, lakini sasa hali inabadilika. 

"Mafanikio haya sasa yako hatarini. Janga la COVID-19 limekuwa tishio kubwa zaidi kwa maendeleo kwa watoto katika historia yetu ya miaka 75. Wakati idadi ya watoto walio na njaa, walio nje ya shule, walionyanyaswa, wanaoishi katika umaskini au kulazimishwa kuolewa ikiongezeka, idadi ya watoto wanaopata huduma za afya, chanjo, chakula cha kutosha na huduma muhimu inapungua. Katika mwaka ambao tunapaswa kutazamia mbele, tunarudi nyuma."

Takwimu mbalimbali za jinsi hali ilivyo mbaya zimetolewa katika ripoti hiyo ikiwemo ile inayoonesha watoto zaidi ya milioni 100 wanakadiriwa kuishi katika umaskini wa namna mbalimbali hili likiwa ni ongezeko la asilimia 10 tangu 2019.

"Katika enzi hizo za janga la Corona, kuendelea kuongezeka kwa migogoro, hali ya mabadiliko ya tabianchi kuzidi kuwa mbaya kunahitaji uangalizi wa karibu zaidi wa watoto. Tupo njia panda, tunapofanya kazi na serikali, wafadhili na mashirika mengine ili kuanza kupanga njia yetu ya pamoja kwa miaka 75 ijayo, ni lazima tuwaweke watoto mbele kwenye mipango ya uwekezaji na kuwaweka mwisho katika mstari wa kupunguza miradi yao. Ahadi ya maisha yetu ya baadaye imewekwa katika vipaumbele tunavyoweka katika maisha yetu ya sasa.” Amesisitiza Fore. 

Ripoti hiyo imetoa mapendekezo kadhaa ya kufanya ikiwemo kuwekeza zaidi katika kuwalinda watoto, na kuwapatia lishe bora. 

Audio Credit
Flora Nducha/ Leah Mushi
Sauti
2'9"
Photo Credit
UNICEF/UN0336408/Babajanyan VII