Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakulima wa mpunga nchini Tanzania wajadili mbinu za kuendeleza zao hilo

Wakulima wa mpunga nchini Tanzania wajadili mbinu za kuendeleza zao hilo

Pakua

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO nchini Tanzania kwa kushirikiana na wadau wake watafiti wa mpunga, Tari na IIRI wamewakutanisha baadhi ya wakulima wa mpunga nchini humo wapeane mawazo jinsi ya kuboresha zao hilo ili pamoja na faida nyingine, waweze kuhudumia soko la nchi zinazoizunguka Tanzania.

Diomedes Pastory Kalisa ni Afisa wa FAO ambaye pia anaratibu mradi wa kujenga uwezo na kubadilishana uzoefu unaofadhiliwa na serikali ya Korea. Bwana Kalisa ananza kwa kufafanua lengo kuu la FAO kukutanisha wakulima.

"Huu mkutano wa wadau lengo lake kubwa ni kuangalia katika upande wa sera. Tukiangalia zao la mpunga na kama tulivyokwisha kusikia kwamba Tanzania sasa hivi tunajitosheleza kwenye zao la mpunga lakini tukiangalia utoshelezaji unajitokeza pale ambapo tunaongeza maeneo ya kilimo."

Diomedes Kalisa anaendelea kueleza kuwa FAO haiishii tu katika kuwasaidia wakulima kuzalisha mazao mengi zaidi bali wanajiuliza maswali zaidi na kuyatafutia ufumbuzi

"Kwamba kama tunajitosheleza kwa chakula tunapoendelea kuongeza uzalishaji mchele wetu unaenda wapi? Tunahitaji kuusafirisha kwenda kuwalisha na nchi nyingine majirani ambao wana uhitaji wa mchele. Lakini Je, katika sera zetu kuna mambo rafiki ambayo yanawezesha kuhakikisha haya tunayafikia? Kupata masoko yanayowezekana yanayojitosheleza? Kuhakikisha kuwa zao letu la mpunga linasafirishwa nje? Kwenye sera zetu tunayo mipango rafiki ambayo inaangalia kwa upande wa pembejeo, mbolea, mbegu. Kwa hiyo katika mkutano huu tunaenda kuangalia katika sera zetu.

Na sasa hivi tuna mpango mkakati wa uendelezaji wa zao la mpunga awamu ya pili ambao umainisha mambo mengi haya ya mbegu ya utafiti ya masoko, yote yanaelezwa mule. Lakini lazima tujikite pia katika kuziangalia sera zetu kwamba zinatoa nafasi gani ili tuweze kuona utekelezaji wake huu unaenda kama tunavyofikiria."

Audio Credit
Flora Nducha/ Diomedes Pastory Kalisa
Audio Duration
2'32"
Photo Credit
Photo: FAO/Olivier Thuillier