Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zaleta uhasama baina ya wakulima wavuvi na wafugaji

Mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zaleta uhasama baina ya wakulima wavuvi na wafugaji

Pakua

Wakati Mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya Tabianchi COP26 ukiwa umemalizika mwishoni mwa wiki huko Scotland huku Afrika ikisema haijafanikiwa ilivyotaraji, huko nchini Cameroon mabadiliko ya tabianchi yameleta uhasama baina ya wafugaji, wakulima na wavuvi, sababu kubwa ya ugonvi huo ni mbinu walizobuni za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Leah Mushi na taarifa zaidi.
 Nats…
 “Mvua ni chache sana. Sijui sababu ya mabadiliko ya tabianchi lakini inabidi tubadilike na kuwahifadhi samaki wakati wa kiangazi. Mavuno tunayapata kwenye kilimo hayatoshi.” Ndivyo anavyosema  Assiam Yere, mkimbizi wa ndani eneo la Musgum nchini Cameroon.

Katika kutafuta suluhu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wakulima na wavuvi wa Musgum wakaona ni vyema kuchimba mashimo makubwa kwa ajili ya kuhifadhi maji ya mvua ili yawasaidie kipindi cha ukame.
 
Lakini wafugaji waarabu wa Choa hawataki kuyaona wala kuyasikia sababu kwao ni mitego ya kifo kwa ng'ombe wao kwani huteleza kwenye miteremko mikali, huvunja miguu na wakati mwingine kuzama kabisa katika mashimo hayo.
 
Robert Mati ni mkulima wa kijiji cha Missiska anasimulia mapigano yaliyotokea mwezi Agosti mwaka huu kati ya wafugaji na wavuvi yalisababisha vifo vya watu 45 na majeruhi 74 . Vijiji 19 viliteketezwa kwa moto na zaidi ya watu 23,000 walilazimika kuyakimbia makazi yao.
“Waarabu wa Choa walikuja kufukia mashimo tuliyochimba. Kwa kweli, walitaka tuyajaze mchanga mashimo siku hiyo hiyo. Ikiwa hatukufanya hivyo walisema wangetuua”
 
Naye mwanakijiji wa kijiji cha  Demza Issa Mahmat, anasema "Kwa sasa, kila mtu anaogopa, usiku ukiwa kitandani, hakuna kulala, wengine wanalala nje."
 
Hofu hii ndio imesababisha maelfu kuyakimbia makazi yao, kuvuka mto Logone hadi nchini Chad. Na ndani ya miezi miwili, takriban watu 8,800 wamesajiliwa kuwa wakimbizi na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhdumia wakimbizi - UNHCR.

Juhudi za UNHCR zimewezesha zaidi wakimbizi wa ndani 12,000 kurejea makwao ingawa wengi wao wanasema hawalali fofofo.

Kwa mujibu wa UNHCR mabadiliko ya tabianchi yamekuwa chanzo kikuu cha watu kuyahama makazi yao na sababu kuu inayowazuia watu kurudi. Wakimbizi wengi wanasema watakabiliwa na njaa ikiwa watarudi nyumbani.

Audio Credit
Assumpta Massoi / Leah Mushi
Audio Duration
2'44"
Photo Credit
CIFOR/Ollivier Girard